Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa amewaagiza makandarasi wanaojenga mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kuhakikisha wanakamilisha mradi huo ifikapo Novemba mwakani.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi na ulaziji wa mabomba katika miji ya Tabora, Nzega na Igunga utakaogharimu kiasi cha Sh. 600 Milioni, Prof. Mbarawa amesema wananchi wanahitaji maji kwa kuwa wameteseka na kuhangaika kwa muda mrefu.
Waziri huyo amewataka makandarasi hao kuhakikisha wanakamilisha mradi huo kwa wakati licha ya muda wa mkataba huo kufikia tamati kuwa Februari mwaka 2020.
“Wananchi wa mkoa wa Tabora wana hamu kubwa ya kuona mradi huu ukikamilika hata kesho, lakini tuhakikishe umekamilika Novemba mwakani,” Amesema Profesa Mbarawa.
Akizungumzia agizo hilo, Meneja Mradi wa Afcons JV, Dhaval Soni amesisitiza watafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanamaliza mradi kama alivyoagiza Waziri Mbarawa.