Home VIWANDAMIUNDOMBINU TEHAMA kuibua fursa za ajira na maendeleo kiuchumi

TEHAMA kuibua fursa za ajira na maendeleo kiuchumi

0 comments 230 views

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amewataka wadau wa TEHAMA kuwapa nafasi watu wa makundi maaluum katika maboresho ya teknolojia kwa kusikiliza maoni yao.

Waziri Nape amesema hayo katika kongamano la saba la TEHAMA linalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 16 hadi 20, 2023 katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC).

Amesema serikali imeingia makubaliano na serikali ya India katika kuboresha TEHAMA hivyo wanapaswa kutumia fursa ya makubaliano hayo katika kujijengea uwezo na kupata uzoefu ili kuifanya nchi kuwa kitovu cha teknolojia bunifu.

“Kama mnavyofahamu wiki iliyopita Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan alifanya ziara huko nchini India ambapo ameonyesha nia thabiti ya kuipeleka nchi hii katika jamii iliyobadilika yenye misingi ya maarifa itakayoifanya nchi kufikia mapinduzi ya nne na ya tano ya viwanda.

Wizara yetu, imesaini mkataba wa mashirikiano na Wizara ya maswala ya kielektroniki ya India kushirikiana kwenye kubadilishana ujuzi na utaalamu wa teknolojia mbalimbali za kidigitali, ubunifu pamoja na teknolojia hizi ibukizi,” ameeleza Waziri Nape.

Amewasihi Watanzania kutumia fursa ya makubaliano hayo kujenga uwezo na kupata uzoefu ili kuweza kuifanya Tanzania kitovu cha teknolojia bunifu kwa ukanda wa Afrika Mashariki na hata bara la Afrika.

Amesema mafanikio hayo yanalenga kufikia maono yalionyeshwa kwenye mkakati wa uchumi wa kidigitali ambao umeandaliwa na Wizara kwa kushirikiana na ofisi za umma na binafsi ambapo mkakati huo upo kwenye hatua za mwisho kupelekwa kwenye maamuzi.

“Hadi sasa, Tanzania imeorodheshwa kwenye ripoti ya Benki ya Dunia (WB) ya ukomavu wa matumizi ya teknolojia kuwa ni ya kwanza kati ya nchi za Afrika Mashariki na yapili kwa bara la Afrika,” ameeleza.

Aidha Nape ameongeza kuwa kufanya ushirikiano na nchi zilizopiga hatua kutasaidia kuiwezesha nchi kusonga mbele kwenye matumizi ya teknolojia.

“Tunayo kila sababu ya kufanikiwa kwenye TEHAMA kwani mazingira tuliyonayo, miundombinu, utashi wa kisiasa uliopo na uwekezaji uliowekwa kwenye miundombinu hatuna sababu ya kubaki nyuma” amesema.

Amesema matumizi ya teknolojia inayoibukia inawezeshwa pamoja na miundombinu rafiki ambapo serikali inatambua juhudi zinazofanywa na sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu hiyo ya mawasiliano.

Amebainisha kuwa “hivi karibuni tumesaini leseni nne za data centers hii inaonyesha ni kwa jinsi gani wawekezaji wanarizika na mazingira yaliyowekwa nchini katika kuhakikisha sekta ya TEHAMA inakua na ongezeko lake linaenda kugusa maisha ya watu”.

Ameeleza kuwa kongamano hilo limezingatia ushiriki wa makundi yote ikiwemo vijana na wanawake.

“Nimeona kwenye majadiliano mmeweka siku maalumu kwa ajili ya wanawake na vijana hii ni nzuri kwani ripoti ya Dunia inaonyesha ushiriki wa wanawake kwenye TEHAMA ni mdogo basi kongamano lijalo muangalie namna ya kuwahusisha watu wenye makundi maalum wakiwemo walemavu,” amesema.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter

Subscribe my Newsletter for new blog posts, tips & new photos. Let's stay updated!