Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) ina mpango wa kujenga gati maalumu kwa ajili ya meli za kitalii kwa lengo la kutoa huduma mbalimbali ikiwemo kupokea maofisa uhamiaji, vyombo vya fedha na taasisi nyingine zinazojihusisha na mapokezi ya meli za kitalii. Hayo yameelezwa na Meneja wa Bandari ya Dar es salaam, Freddy Liundi wakati wa hafla fupi ya kupokea meli ya kitalii iliyokuwa na watalii zaidi ya 400.
“Mamlaka ina mipango ya muda mrefu na muda mfupi ili kuhakikisha tunakuwa na uwezo wa kupokelea meli za watalii katika eneo na gati maalumu ya kupokelea meli za aina hiyo” ameeleza Meneja huyo.
Liundi amesema kuwa hivi sasa, wanakamilisha ujenzi wa gati mpya kwa ajili ya kushusha magari (RoRo). Pamoja na hayo, gati hiyo pia itakuwa na uwezo wa kupokea meli zenye urefu wa zaidi ya mita 300.
“Duniani kuna meli kubwa na ndefu za kitalii, kitu muhimu gati ambayo tunaenda kuikamilisha itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli ya mita 350. Meli ya urefu huo ni kubwa sana kwani ina uwezo wa kubeba watalii elfu nne mpaka elfu tano kwa wakati mmoja. Katika mipango ya muda mfupi kuanzia Septemba mwaka huu tutakuwa na uwezo wa kupokea meli zenye ukubwa huo”. Amesema Meneja huyo.