Na Mwandishi wetu
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es salaam (DAWASA) Romanus Mwang’ingo amesema mamlaka hiyo inatarajia kutumia kiasi cha Sh. 1.3 trilioni ili kujenga miradi mitatu ya kukusanya, kusafisha na kuondoa majitaka katika maeneo mbalimbali hapa jijini.
Mwang’ingo ameeleza kuwa miradi hiyo itaongeza kiwango cha kusafisha majitaka kutoka asilimia 10 zilizopo hivi sasa hadi kufika asilimia 30 mwaka 2020. Ameongeza kuwa mradi wa kwanza utajengwa eneo la Jangwani na utakusanya majitaka kutoka Ubungo, Mwananyamala, Kinondoni, Ilala na Msasani.
Ameongeza kuwa katika awamu ya kwanza ya mradi huo, bomba linalomwaga majitaka baharini litaacha kutumika. Badala yake, mtambo unaojengwa kwa ushirikiano na serikali ya Tanzania na Korea Kusini kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya Korea utatumika ili kusafisha majitaka hayo.