Shirika la Simu la TTCL linatarajia kuanza kutoa huduma ya tiketi za mabasi yaendayo kasi (Udart) baada ya kushinda zabuni na kuingia mkataba na mradi huo. Kwa mujibu wa maelezo ya Ofisa wa Operesheni wa TTCL Pesa, Fatuma Bali, Shirika hilo linatarajia kuanza kutoa huduma hiyo mara baada ya taratibu za kuunganisha mifumo ya malipo kukamilika.
Bali ameeleza kuwa, hivi sasa TTCL wapo katika hatua za mwisho za kuanza mchakato wa utoaji huduma hiyo ambapo inasemekana kuwa mbali na mteja kupata tiketi kwa njia ya kielektroniki, mteja na mtumiaji wa mtandao wa TTCL pia ataweza kupata huduma hiyo kwa kupitia simu ya mkononi ili kurahisisha huduma na vilevile, kuendana na kasi ya teknolojia.
Mradi wa mabasi yaendayo kasi ulianza rasmi jijini Dar es salaam mwaka 2016 na umekuwa ukitumia mfumo wa kielektroniki wa utoaji tiketi lakini hivi sasa tiketi za kawaida zimekuwa zikitumika kutokana na mtoa huduma wa hapo awali, MaxMalipo kumaliza mkataba wake.