Mkuu wa mkoa wa Pwani Evarist Ndikilo ameagiza watumishi walioisababishia Halmashauri ya Mkuranga hasara ya takribani Sh. 500 milioni kwa kujenga nyumba katika makazi yasiyofaa kuchukuliwa hatua. Akizungumza kuhusu sakata hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Mshamu Munde amedai nyumba hizo sita zimejengwa tangu mwaka 2006 lakini watumishi waliopaswa kuzitumia wameshindwa kufanya hivyo kutokana na miundombinu kuwa mibovu hasa katika misimu ya mvua ambapo maji hujaa hadi kuingia ndani.
“Nyumba zipo sita, tatizo kubwa ni kujengwa katika mkondo wa maji, mvua zinaponyesha maji huzingira nyumba hizo na kuingia ndani”. Amefafanua Munde.
Ndikilo ametangaza kuwachukulia hatua wote waliohusika katika mradi huo ambao umepelekea serikali kupata hasara ya mamilioni ya fedha kutokana na ujenzi huo kufanyika katika maeneo ambayo hayafai kwa makazi ya watu.
“Ifunguliwe hoja ili kuokoa fedha za serikali, haiwezekani mamilioni ya fedha yapotee na waliohusika katika hasara hiyo wasichukuliwe hatua”. Amesema Mkuu huyo wa mkoa.