Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar, Dk. Sira Ubwa Mamboya amesema mara baada ya jengo jipya la abiria katika Uwanja wa ndege wa Zanzibar kukamilika,ajira takribani 400 zitapatikana. Dk. Mamboya amesema hayo baada ya kutembelea mradi huo wa ujenzi ambapo ametangaza kuwa vijana watapewa kipaumbele katika ajira hizo.
Waziri huyo ameongeza kuwa serikali ya Zanzibar imejipanga kuwapa elimu vijana ili kuwaandaa na uhitaji wa huduma zinazotolewa hapo kwani wanategemea mashirika makubwa ya ndege kuanza kutua visiwani humo baada ya ujenzi huo kumalizika hivyo fursa ni fursa nzuri ya kukuza utalii.
Kwa upande wake, Mratibu wa jengo hilo, Yasser Decosta amesema ujenzi huo unaohusisha sehemu ya kuegesha ndege, magari pamoja na bustani utagharimu Dola za Marekani 128 milioni na unatarajiwa kukamilika Januari 2019.