Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imetangaza bei mpya za mafuta kwa mwezi Julai ambao bei ya dizeli imeongezeka kwa Sh. 166 huku ile ya petroli ikiongezeka kwa Sh. 126. Ongezeko hilo linatajwa kuwa kubwa zaidi kuwahi kutokea kwa mara moja tangu Agosti 2015 ambapo lita moja ya petroli iliuzwa kwa Sh. 2290 huku ya dizeli ikiuzwa kwa Sh. 2026.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ewura, lita moja ya petroli kwa jiji la Dar es salaam itauzwa kwa Sh. 2409 na ya dizeli itakuwa Sh. 2329. Taarifa hiyo inabainisha kuwa hali itakuwa mbaya zaidi katika mikoa ya Kagera, Geita, Songwe, Tabora, Dodoma, Iringa na Pwani.
Halikadhalika, ongezeko hilo la bei halitaathiri mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha kutokana na bandari ya Tanga kutoingiza shehena mpya ya mafuta hivyo watumiaji wataendelea na bei zilezile za Juni.
Kwa upande wa mafuta ya taa, bei zimetajwa kubaki kama ilivyokuwa mwezi uliopita kutokana na kutoingizwa kwa shehena mpya ya mafuta nchini kupitia bandari ya Dar es salaam.