Home VIWANDANISHATI Dkt. Biteko ataka mitungi gesi ya kupikia ifike ngazi ya vijiji

Dkt. Biteko ataka mitungi gesi ya kupikia ifike ngazi ya vijiji

0 comment 34 views

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Kampuni zinazohusika na Usambazaji wa Gesi za Mitungi Tanzania (LPG) -TZLPGA ambapo wamejadili masuala mbalimbali ikiwemo kufikisha mitungi ya gesi ya kupikia hadi ngazi ya vijiji.

Mazungumzo hayo yamefanyika Februari 20, 2025 jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba pamoja Watendaji kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA) pamoja na Wakala wa Nishati Vijijini ( REA).

Dkt. Biteko amezitaka kampuni hizo kuhakikisha huduma ya upatikanaji wa mitungi ya gesi inafika kwa wingi hadi ngazi ya vijiji ili kuweza kufikia lengo la kuhakikisha kuwa asilimia 75 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2030 ikiwa pia ni utekelezaji wa Mpango wa Mahsusi wa Nishati ( Energy Compact uliosainiwa mwezi Januari 2025.

“Ili Serikali ifanikiwe lazima kuwashirikisha watu wake, tunawashukuru sana kwa mchango wenu katika kufanikisha Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia ambao tangu tuuzindue mwaka 2024, uelewa na matumizi ya mitungi ya gesi umeendelea kuongezeka, mitungi hii ni gharama lakini ninyi mnajitoa na kutuunga mkono,” amesema Dkt. Biteko.

Amesema kuwa lengo la kikao hicho pia lilikuwa ni kujadili changamoto ambazo kampuni hizo wanakutana nazo ikiwemo za kikodi ambazo zina nafasi ya kujadiliwa katika Muswada wa Masuala ya Fedha utakaosomwa katika Bunge la Bajeti la mwaka 2025/2026.

“Tumekutana hapa ili tunapoelekea kwenye Bajeti ya Serikali mtuambie kipi tukiboreshe kupitia Muswada wa Masuala Fedha na ni vizuri pia mkatueleza jambo gani lifanyike ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi,” ameeleza Dkt. Biteko.

Kuhusu Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia amesema kuwa, “tangu tulipozindua Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia tumepata ushirikiano mkubwa sana Afrika na duniani kote kupitia diplomasia ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na tumeendelea kupata fursa kubwa ya kuonesha na kuuelezea  Mkakati wetu, pia tunaalikwa na nchi mbalimbali hata ambazo zimepiga hatua kuliko sisi,  hii inaonesha kwa vitendo dhamira yetu ya kuhakikisha watu wanahama kutoka kwenye matumizi ya kuni na mkaa na kwenda kwenye nishati safi ya kupikia,” amebainisha Dkt. Biteko.

Amesema mwaka 2021 idadi ya watumiaji wa Nishati Safi ya Kupikia nchini ilikuwa asilimia 9 pekee. Aidha, wakati Mkakati huo unazinduliwa Mei 2024 hadi  Februari 2025 watumiaji wamefikia asilimia 33  hivyo ni hatua nzuri katika kufikia lengo la Serikali la kufikisha asimilia 80 ya watumiaji wa Nishati Safi ya Kupikia ifikapo mwaka 2034.

Ameeleza kuwa changamoto inayoikabili Serikali katika kuhamasisha wananchi kutumia Nishati Safi ya Kupikia ni uwepo wa nishati mbadala ambazo si safi za kuni na mikaa ukilinganisha na nchi zingine ambazo hazina urahisi wa upatikanaji wa kuni na mkaa.

Ametaja mbinu ya kukabiliana na  changamoto hiyo kuwa ni kuendelea kutoa elimu mara kwa mara ili kusaidia wananchi kubadili  tabia na mitazamo juu ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.

Akijibu baadhi ya hoja za wajumbe wa Jumuiya hiyo, hususan kuhusu ombi la unafuu wa kodi katika bidhaa za gesi, amesema suala hilo limepokelewa na litafanyiwa kazi na Serikali.

Vilevile, ameishauri Jumuiya hiyo kutumia vyombo vya habari kwa ajili ya kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya Kulipia.

Aidha, ametoa changamoto kwa Jumuiya hiyo kutumia fursa ya Bandari kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji wa mitungi ya gesi katika Ukanda wa Afrika Mashariki ambayo ni faida ya kichumi kwa nchi na pia kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felschemi Mramba amesema kuwa  Serikali inaendelea na mikakati ya kuwa hifadhi maalum za mafuta ambapo suala la hifadhi maalum ya mitungi ya gesi linaangaliwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa  TZLPGA Hamisi Ramadhani amemshukuru Dkt. Biteko kwa kuitisha  kikao na Jumuiya hiyo ili kujadili masuala ya kiutendaji ambayo yanalenga kuhakikisha kampuni hizo zinaendelea kufanya biashara kikamilifu na gesi ya mitungi inapatikana katika maeneo yote nchini kwa wakati wote.

Ramadhani amesema kuwa, kampuni zinazohusika na usambazaji wa mitungi ya gesi zinapata ushirikiano mzuri kutoka Serikalini kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA) kwa kutengeneza sheria zinazoongoza biashara ya LPG,  Wakala wa Nishati Vijjini (REA) kwa kutekeleza programu mbalimbali za Nishati Safi ya Kupikia na Shirika la Viwango Tanzania ( TBS) kwa kuweka viwango (standards) zinazoongoza biashara ya LPG.

Ameipongeza  EWURA pia kwa kuwa mdhibiti bora kwani mara zote imekuwa ikisikiliza maoni ya wadau na kuyafanyia kazi kwa  maslahi ya pande zote mbili ambazo ni Serikali na wafanyabiashara.

Ameongeza kuwa mitungi ya gesi imesambaa sana sehemu za mijini kuliko vijijini hata hivyo kampuni hizo zinajitahidi ili biashara hiyo iendelee kushamiri maeneo ya vijijini.

Katika hatua nyingine, Jumuiya hiyo imesema ipo tayari kushirikiana na Serikali ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji wa LPG katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter