Home VIWANDANISHATI Jinsi ya kubana matumizi ya umeme

Jinsi ya kubana matumizi ya umeme

0 comment 154 views

Gharama kubwa ya umeme imeendelea kuwa kilio kwa wengi ila wanaoathirika zaidi ni vijana ambao ndio kwanza wanaanza kujitegemea. Muda mwingine matumizi ya nishati hii yanaweza kupelekea kuharibu bajeti yako na hata kufikia hatua ya kukopa kwa ndugu au marafiki . Hii haimaanishi kuwa tatizo hili halina suluhisho. Kuna njia rahisi za kudhibiti matumizi yako ya umeme ili kuokoa gharama na kuepuka kutumia fedha nyingi.

Hizi hapa ni baadhi tu ya mbinu rahisi za kubana matumizi yako ya umeme.

Tumia taa za umeme mdogo

Siku hizi kuna aina mbalimbali za taa lakini hii haimaanishi kuwa zote zinafaa kwa ajili ya matumizi yako. Bulb za zamani hutumia umeme mwingi zaidi ikiinganishwa na mpya. Wakati unanunua taa, hakikisha unatafuta ‘Energy Savers’ ambazo zimetengenezwa kwa kutumia teknolojia ambayo inaokoa nishati.

Fahamu mfumo wako wa umeme

Mfumo duni unaweza kuwa chanzo cha umeme mwingi kupotea. Ni vizuri kumshirikisha mtaalamu wa masuala ya umeme kukagua mfumo ulionao na kuhakikisha haukupotezei umeme. Kama umeme unavuja kimakosa na kuingia kwenye waya wa ardhini, umeme mwingi utapotea pasipo wewe kujua.

Zima vifaa vya umeme unapomaliza kutumia

Chanzo kikubwa cha umeme kupotea huwa ni kuacha vifaa mbalimbali vikiwa vimewashwa japokuwa havitumiki kwa wakati huo. Katika mazingira yetu, tumezoea kuacha vifaa kama taa, redio, televisheni au kompyuta vikiwa vimewashwa mchana au usiku kucha bila sababu ya msingi. Weka mazoea ya kuzima vifaa vyako vya umeme ili kubana matumizi.

Changamkia nishati mbadala

Walio wengi wanadhani kwamba wanapotumia umeme kwa ajili ya vitu kama kupikia ndiyo kuwa wa kisasa zaidi. Ukweli ni kwamba unajiongezea gharama ambazo ungeweza kuepuka. Kwenye majukumu kama mapishi, unaweza kutumia nishati ya gesi kwa kuwa ni gharama nafuu zaidi. Pia kwenye vitu vingine, unaweza kutumia umeme wa jua (Solar) ili kuondoa gharama kubwa katika umeme.

Tumia fridge (jokofu) vizuri

Fridge ni moja kati ya vifaa ambavyo vinatumia kiwango kikubwa cha umeme hivyo kwa kupunguza matumizi yake unabadili kiwango cha matumizi ya umeme. Unaweza kuwasha fridge lako kwa muda fulani tu. Pia unaweza kuepuka kulifungua mara kwa mara ili kutunza ubaridi uliopo.

Tumia pasi vizuri

Asilimia kubwa ya umeme hupotea wakati wa zoezi hili. Kunyoosha nguo ni jukumu ambalo kwa sababu mbalimbali hatuwezi kuliepuka lakini matokeo yake kwenye matumizi ya nishati siyo mazuri. Ili kuokoa matumizi katika hili, unashauriwa kununua pasi yenye viwango na ubora stahiki. Vilevile badala ya kunyoosha nguo kila siku, jitahidi kunyoosha kwa pamoja kwani umeme unaotumika kwa pamoja ni mdogo ikilinganishwa na ule utakaotumika kunyoosha nguo moja moja kila siku. Mbali na hayo, inashauriwa kunyoosha wakati kuna umeme wa kutosha ili pasi isivute sana umeme na kupelekea matumizi makubwa.

Tumia feni/AC vizuri

Watu wengi hupenda kutumia feni au AC ili kupambana na hali ya hewa ya joto.  Unachotakiwa kufahamu ni kwamba, vifaa hivi (hususani AC) huhitaji umeme mwingi ili kujiendesha.

Ili kuhakikisha kuwa hutumii umeme mkubwa katika hili, unaweza kutumia mbinu mbadala kupambana na joto kama vile kufungua madirisha hasa ikiwa mchana ili kuruhusu upepo kuingia ndani kwa wingi. Ikiwa umewasha AC, hakikisha umefunga madirisha na milango ili kupata baridi haraka na hakikisha vifaa hivi vinazimwa ikiwa havihitajiki.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter