Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) wakiongozwa na Makamu Mwenyekitii Ndugu Japhet Hasunga walifanya ziara kwenye mradi wa makaa ya mawe wa Kiwira ambapo kamati ilitembelea maeneo mbalimbali ya mgodi ikiwemo mradi wa kutengeneza nishati mbadala ya Rafiki Briquette.
Katika ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Deusdedith Magala aliwaongoza wajumbe wa kamati kushudia shughuli mbalimbali zinazofanywa mgodini hapo zikiwemo uchimbaji na uchakataji wa makaa ya mawe na mradi wa Rafiki Briquette.
Aidha Wajumbe wa Kamati walipongeza mageuzi na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Shirika katika mgodi wa Kiwira .
Wajumbe pia waliridhishwa na maendeleo ya mradi wa nishati safi ya kupikia ya Rafiki Briquette na kusisitiza nishati hiyo muhimu iweze kuwafikia wananchi wengi ili kuendelee kuunga mkono ajenda ya upatikanaji wa Nishati safi kwa Watanzania
Aidha Naibu Waziri wa Madini Dkt Steven Kiruswa ambae aliambatana na Kamati katika ziara hiyo aliishukuru kamati kwa maoni yao na miongozo mbalimbali wanayoitoka kwa Shirika ambayo imeleta mafanikio makubwa mgodini hapo.
Kabla ya Ziara hiyo ya Kiwira kamati iliweza kupata wasilisho la Utekelezaji wa Shughuli za Shirika tarehe 06.03/2025 Jijini Dodoma katika semina iliyoongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Eng Yahya Samamba.
Katika semina hiyo kamati ililipongeza STAMICO kwa mageuzi makubwa yaliyofanywa na Shirika katika kipindi kifupi na kuwataka kuongeza juhudi zaidi ili kuongeza mapato ya Shirika.