Waziri wa Nishati Dk. Medard Kalemani amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa kusambaza umeme vijijini (REA) pamoja na wakandarasi wote nchini kusitisha uagizaji wa vifaa nje ya nchi ifikapo Novemba mwaka huu na badala yake, watumie vifaa vinavyozalishwa hapa nchini ili kuokoa gharama pamoja na muda wa utekelezaji wa miradi husika.
Dk. Kalemani ametoa agizo hilo jijini Dar es salaam wakati wa ziara yake katika kiwanda cha Auto Mech ambacho kinazalisha vifaa vya miundombinu ya umeme, ikiwa ni miezi mitatu tu tangu serikali kupiga marufuku uagizaji wa mita za umeme kutoka nje ya nchi ili kuvijengea uwezo viwanda vya ndani na kubana matumizi.
Kalemani ametoa wito kwa kiwanda hicho kuongeza uzalishaji kwa tani kumi na tano kwa siku badala ya tani tano ili TANESCO iweze kuongeza kasi ya kuhudumia wananchi. Naye Mmiliki wa kiwanda hicho Ramesh Patel amemueleza Waziri Kalemani kuwa, uzalishaji utazingatia ubora wa viwango vya TBS ili kuhakikisha usalama wa vifaa hivyo.