Home VIWANDANISHATI Tanzania yaikaribisha kampuni za China kuwekeza Sekta ya Nishati

Tanzania yaikaribisha kampuni za China kuwekeza Sekta ya Nishati

0 comment 142 views

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian ambapo wamezungumza masuala mbalimbali ikiwemo uhusiano uliopo kati ya Tanzania na China na uwekezaji kwenye miradi ya Nishati.

Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam Novemba 24, 2023 na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Ubalozi wa China nchini Tanzania wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba.

Dkt. Biteko amemweleza Balozi Mingjian kuwa Tanzania inathamini uhusiano mzuri ulipo kati ya nchi hizi mbili ambao mwakani utafikia miaka 60 huku akitaja miradi mbalimbali kwenye Sekta ya Nishati na Madini ambapo kuna Wawekezaji na Wakandarasi kutoka China.

“Sisi Tanzania tunaufurahia na kuuthamini uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi yetu Tanzania na China, na hapa kuna kampuni nyingi kutoka China zinazofanya kazi kwenye uchimbaji madini ikiwemo madini ya viwandani na uchenjuaji madini.

Pia kwenye miradi ya Nishati kuna kampuni za Kichina zinafanya kazi mfano kampuni ya TBEA inayojenga laini ya umeme ya kV 400 kutoka Chalinze hadi Dodoma, na mradi wa kusafirisha umeme wa kV 400 kutoka Tanzania kwenda Zambia,” ameeleza Dkt. Biteko.

Kuhusu miradi hiyo ya usafirishaji umeme kutoka Chalinze hadi Dodoma na mradi wa TAZA, Dkt. Biteko ametoa wito kwa Serikali ya China kuiwezesha kwa namna mbalimbali kampuni hiyo ikiwemo kifedha ili itekeleze miradi hiyo kwa ufanisi na kwa wakati kutokana na umuhimu wa miradi hiyo.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa, nchi ya Tanzania bado ina uhitaji wa umeme utakaotokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo maji hivyo amekaribisha kampuni kutoka China kuja kuwekeza kwenye eneo hilo.

Dkt. Biteko amemweleza pia Balozi Mingjian kuhusu mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ambapo ameeleza kuwa nchi ya Uganda na Tanzania zinauthamini mradi huo na zinaendelea na utekelezaji wake ambapo kampuni kutoka China ya CNOOC ni moja ya Wabia wa mradi huo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter