Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kapuulya Musomba amesema shirika hilo linafanya mazungumzo na DART ili kuwezesha mabasi yaendayo kasi takribani 300 kutumia nishati ya gesi asilia. Musomba amesema hayo jijini Dodoma wakati wa semina ya siku mbili ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini na kueleza kuwa, hadi sasa, zaidi ya magari 200 yanatumia nishati hiyo na kwamba tayari kuna kituo kimoja maalum kwa ajili ya kujaza gesi kwenye magari.
“Mazungumzo yetu na DART yanaendelea vizuri, tunataka mabasi zaidi ya 300 ya mwendokasi ambayo yanatarajiwa kuingizwa nchini yatumie gesi asilia, na hii imeonekana kuwa itawasaidia kupunguza gharama za mafuta kwa wastani wa asilimia 40”. Amesema Kaimu huyo.
Pamoja na hayo, Musomba pia amezungumzia mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mradi wa gesi iliyoshindiliwa (CNG) jijini Dar es salaam na kusema tayari nishati hiyo imeunganishwa katika nyumba 96, na wanalenga kufikia nyumba 212 hadi Juni mwaka huu.
“Lengo ni kufikia jumla ya nyumba 212 kwa mkoa wa Dar es salaam ifikapo Juni mwaka huu, na kwa upande wa mkoa wa Mtwara vibali vyote vya wilaya, mkoa na serikali za mitaa na vijiji zimepatikana na lengo letu ni kuunganisha nyumba 125 na taasisi nne”. Amesema Musomba.