Mkuu wa mkoa wa Geita Robert Gabriel amesema takribani makampuni 100 yamejitokeza na kushiriki maonyesho ya teknolojia ya dhahabu ambayo yatafanyika mkoani humo kwa mara ya kwanza. Maonyesho hayo yatakayofanyika kila mwaka ni hatua mojawapo ya mkoa huo kuwakutanisha wachimbaji wakubwa, wadogo na wa kati pamoja na wadau mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara na jumuiya nyingine ili kujadili mbinu bora za uzalishaji wa dhahabu.
Waziri wa Madini Angellah Kairuki atafungua maonyesho hayo yatakayofungwa jumapili ijayo na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa. Kwa mujibu wa Mkuu wa mkoa huyo, baadhi ya makampuni 1000 yaliyojitokeza hadi sasa ni pamoja na yale ya uchimbaji, ulinzi na huduma za kifedha zikiwemo Geita Gold, Acacia, Suma JKT na NBC.
“Makampuni zaidi ya 250 yalidhibitisha kuwa yatashiriki na mpaka sasa ni baadhi tu yamewasili kwa ajili ya maonyesho, hivyo hakuna shaka kuwa yatakwenda vyema, kwani ni maonyesho ya aina yake kufanyika nchini”. Amesema Gabriel.
Katika maonyesho hayo, mada zitakazopewa kipaumbele ni uchumi, uwekezaji, ujasiriamali, huduma za kijamii pamoja na madini ya dhahabu. Mkuu huyo wa mkoa ametoa wito kwa wakazi wa Geita kujitokeza kwa wingi kwani ni kwa ajili ya maendeleo yao.