Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amepiga marufuku utengenezaji, uingizaji na matumizi ya mifuko ya plastiki kwa shughuli mbalimbali kuanzia Juni mosi mwaka huu. Waziri Majaliwa amesema hayo bungeni Dodoma wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2019/2020.
“Hivi karibuni nimemuagiza Waziri anayesimamia masuala ya mazingira ikiwemo kuzungumza na wadau mbalimbali, ikiwemo wenye viwanda vya kutengeneza mifuko ya plastiki kwa ajili ya kuhakikisha jambo hili linatekelezwa kwa haraka. Kuanzia sasa tunatoa fursa ya viwanda kubadilisha teknolojia, wauzaji kuondoa mzigo uliopo, Ofisi ya Waziri wa Nchi, Makamu wa Rais itajiandaa kutumia kanuni chini ya Sheria ya Mazingira ili kulifanya katazo hili kuwa na nguvu ya kisheria. Tunachukua hatua hii ili kulinda afya ya jamii, wanyama, mazingira na miundombinu dhidi ya athari kubwa zinazotokana na taka za plastiki”. Ameeleza Waziri Mkuu.
Aidha, Majaliwa ameweka wazi kwamba serikali inatambua ni lazima baadhi ya bidhaa zifungwe kwenye vifungashio vya plastiki na kuongeza kuwa, vifungashio kwa ajili ya bidhaa hizo havitapigwa marufuku.
“Kwa msingi huo, katika hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais, yatatolewa maelezo ya kina kuhusu katazo la vifungashio vya aina hii, hasa katika maeneo ya uzalishaji viwanda, sekta ya afya, na kilimo”. Amesema.
Waziri Mkuu amesema mbali na kutunza mazingira, anatarajia kuwa utaratibu huo utaibua fursa za ajira hasa kwa watu wa chini, kupitia utengenezaji wa mifuko mbadala ya plastiki pamoja na vilevile viwanda vya karatasi vilivyopo hapa nchini. Amesisitiza kuwa matumizi ya plastiki yamekuwa na madhara makubwa ikiwemo uchafuzi wa mazingira, vifo vya mifugo, kuziba kwa mifereji na vituo vya kukusanya taka kushindwa kuziozesha.