Home VIWANDAUZALISHAJI Misitu, asali kutumika kama zao jipya la utalii

Misitu, asali kutumika kama zao jipya la utalii

0 comment 83 views

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa ametaka eneo la misitu na asali kufanyiwa utafiti wa kutosha ili litumike kama zao jipya la utalii.

Amewataka watendaji wa sekta ya Misitu na Nyuki kukamilisha mkakati wa kuongeza uzalishaji wa asali kutoka tani 35,000 za sasa hadi tani 138,000 katika kipindi cha miezi miwili.

Waziri Mchengerwa amesema hayo katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyofanyika kitaifa katika Uwanja wa Bombadia mkoani Singida ambapo mkakati huo umepewa jina la “achia shoka kamata mzinga”.

Waziri Mchengerwa amezindua Mwongozo wa Usimamizi wa Hifadhi za nyuki, na vibanda maalum vya kuuzia asali na kutoa Tuzo tano kwa wadau wenye mchango mkubwa kwenye Sekta ya nyuki na vyeti kwa wanafunzi walioandika insha nzuri kuhusu ufugaji wa nyuki.

Akisoma hotuba yake amesema pamoja na uwepo wa maeneo makubwa yaliyohifadhiwa na yanayofaa kwa ajili ya kuzalisha mazao ya nyuki yenye viwango bora bado takwimu zinaonesha uzalishaji ni 23% ikilinganishwa na uwezo uliopo wa kuzalisha tani 138,000 kwa mwaka.

Kutokana na hali hiyo Mchengerwa ameelekeza Wizara ya Maliasili ishirikiane na Wizara ya Kilimo kuanzisha programu za matumizi ya makundi ya nyuki kwenye uchavushaji mimea ili kuweze kuongeza kiwango na ubora wa mazao yanayozalishwa.

Ameitaka Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mfuko wa Misitu kuhakikisha wanawezesha wananchi hasa wale wanaopakana na maeneo ya hifadhi kwa kuwapatia mafunzo ya ufugaji nyuki pamoja na mizinga ya kisasa pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali kuhamasisha jamii kupanda na kutunza miti katika maeneo yao.

Aidha, amesema pamoja na Serikali kuweka jitihada kubwa kwenye kulinda na kuhifadhi maliasili, bado katika kipindi cha hivi karibuni kumekuwa na kasi kubwa ya uharibifu wa maeneo yaliyohifadhiwa kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter