Ikiwa Tanzania ina zaidi ya hekta milioni 48 za misitu, wadau wametakiwa kuchangamkia fursa za kiuchumi zinazotokana na misitu na kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wake.
Hayo yalibainishwa na Mhifadhi Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Dkt. Elikana John, katika kongamano la maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani, lililofanyika Machi 20, 2025, katika viwanja vya Sabasaba, Njombe.

Mhifadhi Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Dkt. Elikana John.
Dkt. John alisema kuwa misitu ni chanzo kikubwa cha fursa za kiuchumi, ikiwa ni pamoja na biashara ya mbao, utalii, uzalishaji wa bidhaa mbalimbali, na ufugaji wa nyuki.
Alisisitiza kuwa misitu inaweza kuwa mkombozi wa uchumi wa Tanzania ikiwa jamii na wadau watajitokeza kwa wingi katika kutunza na kuendeleza rasilimali hii. Alihimiza ushirikiano wa sekta binafsi na wadau wa mazingira katika kuboresha usimamizi wa misitu na kutangaza faida zake kiuchumi.
“Tanzania ina zaidi ya hekta milioni 48 za misitu, ingawa sekta hiyo inakabiliwa na changamoto za ukataji miti holela, mabadiliko ya tabianchi, na upungufu wa mitaji kwa wakulima wadogo na wawekezaji.
Ili kukabiliana na changamoto hizi, TFS inashirikiana na mashirika ya kimataifa kama Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) na Mradi wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) katika kutekeleza miradi ya uhifadhi wa misitu na kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi endelevu,” alisema Dkt. John.
Aidha, Dkt. John alibainisha kuwa Tanzania ina fursa kubwa ya kutumia misitu yake, ikiwa ni pamoja na upandaji wa miti ya kibiashara kama Prunus africana, inayotumika kutengeneza dawa za binadamu, na miti ya mpira, inayozalishwa kwa ajili ya viwanda vya viatu na bidhaa nyingine za mpira.
Dkt. John pia alieleza kuwa mianzi, ambayo inapatikana kwa wingi nchini, inaweza kutumika kutengeneza fanicha, vyombo vya jikoni, na mkaa mbadala wa rafiki kwa mazingira.
Aliongeza kwa misitu ya mikoko, yenye ukubwa wa hekta 158,000 kwenye mwambao wa Bahari ya Hindi, pia inayo fursa ya kukuza utalii wa mazingira, kama ilivyofanikiwa Zanzibar. Dkt. John aliongeza kuwa ikiwa fursa hizi zitachukuliwa, Tanzania inaweza kuwa kinara wa uhifadhi wa misitu barani Afrika.
Katika mwendelezo wa maadhimisho hayo, Dkt. John alihitimisha kwa kusema, “Mtu mmoja, mti mmoja—hili likifanyika kila mwaka, Tanzania inaweza kuwa kinara wa uhifadhi wa misitu barani Afrika.”