Meneja uzalishaji wa kiwanda cha kuzalisha sukari cha Kagera Vicent Mtaki ameishauri serikali kudhibiti uingizwaji holela wa sukari kutoka nje ya nchi unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara ili kukinusuru kiwanda hicho ambacho kinazalisha kwa kiasi kikubwa na kusambaza sukari katika mikoa ya kanda ya ziwa. Mtaki amefafanua kuwa vibali vikiendelea kutolewa na hivyo kuruhusu wafanyabiashara kuendelea kuagiza sukari nje ya nchi, kiwanda hicho kitakosa soko na sukari inayozalishwa itabaki kwenye maghala.
Akizungumzia kuhusu mwenendo wa uzalishaji, Mkuu wa mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti amewataka wakulima mkoani humo kuongeza jitihada katika uzalishaji wa mazao yanayohitajika kwa wingi viwandani katika kuzalisha bidhaa mbalimbali ili kuweka mazingira mazuri kwa viwanda hivyo kupata malighafi. Kwa upande wake, Meneja wa Mfumo wa taifa wa bima ya afya (NHIF) katika mkoa huo, Elius Odhiambo ametoa wito kwa wakulima kuchangamkia fursa na kujisajili katika mfumo huo ili kupata huduma bora.