Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema Serikali ina lengo la kuifanya Tanzania kuwa moja ya mataifa 10 yenye hifadhi kubwa ya dhahabu barani Afrika kwa ustawi wa taifa.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema hayo Januari 22, 2025, jijini Dodoma, wakati akiwasilisha taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, taarifa inayohusu utendaji wa viwanda vya kusafisha dhahabu nchini kwa kipindi cha Machi hadi Desemba 2024 pamoja na mwenendo wa ununuzi wa dhahabu unaotekelezwa na Benki ya Tanzania (BoT).
Akiwasilisha taarifa hiyo, Waziri Mavunde amesema BoT imenunua tani 2.6 za dhahabu inayochimbwa na kusafishwa hapa nchini ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukabiliana na changamoto ya upungufu wa fedha za kigeni, kuboresha akiba ya fedha za kigeni, na kuimarisha thamani ya shilingi ya Tanzania.
Ameeleza kuwa kupitia mpango huo wa BoT, lengo la Serikali ni kuifanya Tanzania kuwa moja ya mataifa 10 yenye hifadhi kubwa ya dhahabu barani Afrika kwa ustawi wa taifa.
Mwenendo wa Ununuzi wa Dhahabu BoT
Kwa mujibu wa Waziri Mavunde, Oktoba 1, 2024, Tume ya Madini ilitoa tangazo linalowataka wachimbaji na wafanyabiashara wa dhahabu kutekeleza takwa la Kifungu cha 59 cha Sheria ya Madini Sura 123, ambalo linawataka kutenga asilimia 20 ya dhahabu na kuiuzia BoT kupitia viwanda vya usafishaji vilivyoidhinishwa.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, Tangu kutolewa kwa tangazo hilo hadi Januari 21, 2025, BoT imefanikiwa kununua tani 2.6 za dhahabu kutoka kwa wachimbaji wa kati, wachimbaji wadogo, na wafanyabiashara wa dhahabu. Thamani ya dhahabu hiyo ni zaidi ya shilingi bilioni 570 kwa mujibu wa bei ya soko la dunia ya tarehe 22 Januari 2025,” ameeleza Mavunde.