Usawa wa kijinsia mahali pa kazi ni muhimu.
Kampeni ya kuimarisha usawa wa kijinsia imeendelea kuwa ajenda kubwa na sasa benki ya NMB imeahidi kuendelea kutekeleza dhamira yake ya kuchochea usawa wa kijinsia katika sekta ya kibenki nchini.
Hayo yameelezwa Septemba 8, 2022 katika mkutano ulioandaliwa na Shirika la International Finance Corporation (IFC) jijini Dar es Salaam kujadili mafanikio ya mradi wa ‘Finance2Equal’ kwa wadau.
Akizungumza kwenye mkutano huo Afisa Mkuu Rasilimali Watu wa NMB, Emmanuel Akonaay amesema kwa muda mrefu wamekuwa mstari wa mbele kudumisha usawa wa kijinsia mahala pa kazi.
Amesema bila ukuaji jumuishi wa kijinsia, kufikia ukuaji wa muda mrefu wa kiuchumi itabaki kuwa ndoto.
“Utafiti unaonyesha kuwa uwiano wa kijinsia unaweza kuchochea ukuaji wa kiuchumi, kuimarisha uchumi na utulivu kifedha na uwiano wa kipato,” amesema.
Amesema tayari benki yake imepiga hatua kubwa katika suala zima la kuongeza uwiano wa usawa wa kijinsia na kusema kuwa katika benki hiyo, uwiano wa kijinsia umepanda kutoka asilimia 45 wanawake, asilimia 55 wanaume mwaka 2015 na kufikia asilimia 49 wanawake, asilimia 51 mwaka huu.
“Ahadi yetu juu uwiano wa kijnsia haishii tu kwa wafanyakazi wetu wa ndani ya benki bali hata kwa wanawake tunaowahudumia kwenye soko letu,” ameeleza.
Amesema mwezi Febuari, 2022 benki hiyo imetoa hati fungani ya kipekee na ya kwanza kutokea kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki almarufu kama ‘Jasiri Bondi’ ambayo ilisaidia upatikanaji wa Sh74.2 bilioni ambazo zitatumika kutoa mikopo nafuu kwa wajasiriamali wanawake au biashara za wanawake na zile ambazo zinagusa wanawake moja kwa moja.
“Ilikuchangia ushiriki wa wanawake kwenye sekta za kilimo, ufugaji, uchimbaji madini na uchumi wa bluu, benki yetu ilitenga Sh100 bilioni kusaidia kuendeleza mnyororo wa thamani kwenye sekta ya kilimo kwa riba isiyozidi asilimia 10 kwa mwaka. Hata hivyo, tuliweza kuchangia Sh100 bilioni za ziada kwa riba ya asilimia 9 kwa mwaka.
Akonaay amesema kwa sasa nchini, wanawake wengi wanakosa fursa za kifedha kutokana na kutengwa na mifumo mingi ya kifedha hali ambayo inaathiri uchangiaji wao kwenye shughuli za kiuchumi.
Awali, Mwakilishi Mkazi wa IFC nchini Tanzania Frank Ajilore amesema uwekezaji kwa wanawake kupitia ajira, uongozi, ubunifu ni muhimu sana na unasaidia kuchochea ukuaji wa uchumi.
“Kwa miaka kadha iliyopita kwa mfano, wateja wetu kutoka taasisi za kibenki 150 ilibaini kuwa mikopo chochefu kwa wanawake ilikuwa asilimia 3.6 tu,” amesema.
Amesema, kwa hapa Tanzania, shirika lake limeendelea kuwezesha wanawake kifedha huku aliongeza kuwa shirika hilo liliwekeza kwenye hati fungani iliyotolewa na beni y NMB ilikudiririsha dhamira yake ya kuwezesha wanawake nchini.