Vodacom Tanzania waongeza ushiriki wa wasichana katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), kupitia mafunzo ya teknolojia ya ku-code yaliyodhaminiwa na kampuni hiyo ambapo awamu ya pili ya mafunzo yalichukua siku tano na kuona wanafunzi 59 wakihitimu mafunzo hayo yaliyofanyika katika taasisi atamizi ya Dar Teknohama Business Incubator (DTBI).
Shirika la Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa linasema, ‘ushiriki wa wanawake katika sayansi na teknolojia ni mdogo ukilinganisha na wanaume. Hivyo Code like a girl ni programu ya kimataifa yenye lengo la kuandaa Wasichana kuwa na ujuzi unaohitajika katika soko la ajira ya technolojia.
Kwa kushirikiana na DTBi, mafunzo haya yalijumuisha elimu ya lugha za kompyuta na utengenezaji wa programu kama HTML, CSS, GitHub and Bootstrap. Mafunzo yalitolewa kwa mfumo wa ushirikiano na yalijumuisha mafunzo ya kijamii pamoja na ku-code ili kuwawezesha kutengeneza tovuti zao wenyewe. Washiriki pia walipewa mafunzo ya kuwasilisha mada na mawasiliano.
“Tumefurahishwa na idadi ya wanafunzi waliohudhuria semina hii, wiki ilifana na mafunzo mbali mbali ya maisha, coding, mawasilisho, pamoja na mafunzo ya ujuzi wa mawasiliano. Mwishoni mwa juma, wasichana walikuwa wamiliki wa tovuti ambazo walitengeneza wao binafsi, “alisema Zaituni Ally, Mkuu wa kitengo kinachoangalia ufanisi wa shirika (Head of Organizational Effectiveness) akimuwakilisha Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Vodacom, Bi Vivienne Penessis.”Leo, mabadiliko ya kidijitali yanatokea kila mahali duniani, kwa hiyo, ni muhimu kuandaa wasichana kwa mabadiliko haya katika soko la ajira,” aliongeza.
Akizungumza kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa DTBi Dr George Mulamula anasema kuwa “Katika awamu ya kwanza ya mafunzo, tuliona kuwa idadi kubwa ya wanafunzi, hasa wasichana katika shule za sekondari wanafundishwa kwa nadharia badala ya vitendo kuhusiana na teknolojia ya Mawasiliano (ICT). Hivyo basi mkakati huu wa mafunzo haya una lengo la kuwawezesha Wasichana nchini kote kupata elimu ya ICT, lakini pia kuwasaidia kupata fursa mbalimbali katika mazingira ya teknolojia kama vile wenzao wa kiume, “aliongeza.
Lengo la Vodacom ni kutoa fursa kwa wasichana nchini kote kushiriki katika masomo ya STEM; kwani “Coding ndio nati na spana za dijitali siku zijazo. Kupitia mipango kama hii, tunatarajia kuona wasichana wengi katika sekta ya Teknolojia. Pia kuwasaidia vijana kupanua ujuzi wao kupitia teknolojia ili Kuleta maendeleo nchini Tanzania “alielezea Bi Zaituni.