Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (NATCOM-Unesco), Profesa Hamisi Malebo amewataka Watanzania kuchangamkia ufadhili wa masomo unaotolewa na shirika hilo ili kutanua uwezo wa rasilimali watu katika nyanja mbalimbali.
Alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki wakati wa kutangazwa kwa mshindi wa tuzo ya kwenda kujinoa zaidi katika utafiti kwa Mtanzania, Doreen Richard Mushi kupitia Mpango wa Masomo wa Kutanua Uwezo wa Utafiti kwa udhamini wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) unaojulikana kama The Unesco/Keizo Obuchi Research Fellowship .
Mtanzania huyo kutoka Chuo Kikuu Huria Tanzania atakwenda Japan na Canada kwa miezi minne kufanikisha utafiti wake juu ya menejimenti ya ufahamu wa data katika Tehama unavyoweza kusaidia mfumo wa kujifunza wa wanafunzi.
Doreen ameibuka mshindi kati ya watu 280 walioomba nafasi hiyo.
Profesa Malebo aliwataka watanzania kutumia nafasi mbalimbali zinazotangazwa kushindaniwa na taasisi yake kutafuta masomo na kwamba taasisi hiyo huchagua kwa haki kwa kuzingatia vigezo na ushindani uliopo.
Alisema kwa sasa watu wengi hawajitokezi kuomba nafasi hizo za ufadhili kupitia Unesco, na kuwataka waombe kwa kuwa nafasi hizo huenda yule anayestahili kwenda kutokana na vigezo vilivyopo ambavyo ni vya kishindani.
“Natoa wito kwa watanzania kutumia nafasi tunazopewa na Unesco kwani ni msaada mkubwa katika kuimarisha na kuboresha elimu na kuwezesha watanzania hasa vijana kupata elimu ya kusaidia kusogeza mbele maisha” alisema Profesa Malabo.
Naye mgeni rasmi katika hafla hiyo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ameishukuru serikali ya Japan kwa kuwezesha Unesco kutoa ufadhili huo muhimu kwa taifa hili.
Akimwakilisha Waziri Ndalichako, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Prof Cuthbert Kimambo alisema kwamba serikali ya Tanzania pamoja na kushukuru Japan kwa kumwezesha Mtanzania huyo, pia inaamini wale waliomaliza mafunzo yao watarejea nchini na kuyafanyia kazi yale waliojifunza na kuleta maendeleo.
Alisema pamoja na kuleta ufanisi katika ubadilishanaji wa maarifa kupitia mafunzo hayo ni matarajio ya serikali kwamba wanaopewa mafunzo hayo watahamisha elimu hiyo kwa wenzao na kulisogeza mbele zaidi gurudumu la maendeleo.
Mpango wa masomo wa kutanua uwezo wa utafiti kwa udhamini wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) unaojulikana kama The Unesco/Keizo Obuchi Research Fellowship ulianzishwa mwaka 2000 na aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Unesco Koichiro Matsura kwa kutafakari maono ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan wakati huo , Keizo Obuchi ambaye aliamini katika uwezo wa watu katika kuibadili na kuijenga dunia hivyo haja ya kujiongezea maarifa zaidi ili kuwepo na maendeleo.
Lengo la programu hiyo ni kuwezesha kuwa na uhakika katika utunzaji wa mazingira, kuleta mazungumzo ya kimataifa na kuendeleza suala la mawasiliano na teknolojia. Programu hii ni matokeo ya ushirikiano kati ya serikali ya Japan na UNESCO katika kuendeleza rasilimali watu kwa nchi zinazoendelea.
Programu hii ambayo ilianzishwa mwaka 2001, imeshawezesha watu 290 hasa vijana watafiti, ambapo 82 wametoka Afrika, kutanua uwezo wao katika nyanja wanazozifanyia kazi.
Miongoni mwa nchi ambazo zimeshanufaika ni Tanzania ambapo katika programu ya mwaka 2014 na 2015, Fatuma Ubwa na Juliana Samuel Kamaghe, walipata nafasi ya kujiimarisha katika sekta ya habari na teknolojia ya mawasiliano.
Doreen Richard Mushi ambaye amekuwa mshindi wa UNESCO/Keizo Obuchi Research Fellowships ya mwaka 2018 alikuwa anashindana na watu wengine 280 na ameshinda katika nyanja ya habari na teknolojia ya mawasiliano (Tehama).
Tuzo hiyo itamwezesha Doreen Mushi kufanya kazi kwa miezi miwili na watafiti wa taasisi ya Learning Analytics Centre ya Chuo Kikuu cha Kyushu nchini Japan, na miezi mingine miwili na watafiti wa kitivo cha elimu, Chuo Kikuu cha British Columbia mjini Vancouver, Canada.
Katika vyuo vyote viwili Doreen Richard Mushi, aliyezaliwa Agosti 27, 1983 atafanya utafiti kuhusu takwimu na uchambuzi utakaosaidia mifumo ya kusoma kwa wanafunzi.