Ni dhahiri kuwa kilimo ni muhimu kwa taifa letu na kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, zaidi ya asilimia 70 ya watanzania wanategemea sekta ya kilimo kujikimu kimaisha. Katika kila biashara masoko ni muhimu ili biashara iendelee. Wakulima wamekuwa na changamoto mbalimbali katika kuuza mazao yao. Moja kati ya tatizo kubwa zaidi ni masoko. Wengi wamekuwa wakipata hasara kutokana na mazao kuharibika baada ya kukaa muda mrefu kwa sababu ya kukosa wateja
Jack Langworthy, mwanzilishi wa App ya “Ninayo” ni miongoni mwa watu wachache ambao wamedhamiria kurahisisha maisha ya wakulima nchini katika upande wa masoko. App hiyo iliyoanzishwa mwaka 2015, imelenga kutoa huduma ya mauzo na manunuzi ya mazao kwa wakulima. Kupitia mtandao huo hakuna gharama kwa mkulima au mnunuzi wakati wa kuweka matangazo ya kununua au kuuza mazao.
Idadi kubwa ya wakulima wapo maeneo ya vijijini na wengi wao hawana uwezo wa kusafirisha mazao yao kwenda katika masoko makubwa, lakini kupitia mtandao huu mkulima ana uhakika wa kunufaika zaidi kupitia mazao yake kutokana na mawasiliano ya moja kwa moja na wanunuzi wa mazao kutoka sehemu mbalimbali.
Pia kupitia programu hii, mkulima anakuwa anajua ni mazao gani yanauza zaidi katika kipindi husika, hivyo kuwapelekea kuzalisha mazao hayo kwa wingi na kujua kiasi kinachohitajika sokoni.
Hadi sasa programu hiyo imeshinda tuzo ya Entrepreneurial Venture Award inayotolewa na Chama cha Wahitimu wa Masomo ya Biashara (AMBA) jijini London. Aidha, imeelezwa kuwa wakulima takribani 20,000 kutoka nyanda za juu kusini wanatumia programu hii kwa ajili ya kutafuta wateja. Mbali na hayo, Ninayo wanaendelea kutangaza programu hii na kuelimisha wakulima kuhusu umuhimu wake kwa ajili ya kupata masoko zaidi.
Kuna umuhimu mkubwa wa kutoa elimu zaidi kwa wakulima na kutoa vifaa ambavyo vinaweza kuwasaidia kufikia programu kama hizi ili kuweza kunufaika na kuondokana na umasikini. Wakulima wengi ni wanachama wa vikundi mbalimbali vya kilimo, hivyo kama kila kikundi kitakuwa na simu au kompyuta itakuwa rahisi kwa wakulima husika kuuza mazao yao kwa bei nzuri na kunufaika. Mbali na serikali, hata taasisi zenye malengo ya kuinua sekta ya kilimo zinaweza kuangalia ni namna gani zinaweza kufanya ili kuhakikisha wakulima nchini wana uelewa wa programu kama hizi na wanakuwa na uwezo wa kuzitumia ipasavyo.