Ikiwa unafikiria kufanya biashara mtandaoni, basi muda muafaka wa kuanza ni sasa. Biashara ya mtandao inaendelea kukua kila siku na soko ni kubwa. Inawezekana unataka kuanzisha biashara lakini hujui ni kitu gani unatakiwa kuuza. Jambo la kujiuliza hapa ni, unachagua vipi bidhaa sahihi? Biashara hiyo itakunufaisha? Ni muhimu kuelewa kuwa aina ya bidhaa inayouzwa ni msingi wa mafanikio yako hivyo unatakiwa kuhakikisha unafanya maamuzi sahihi katika hili.
Unaweza kuwa na wazo zuri lakini unapoingia sokoni bila kufanya utafiti wa kina, unaweza kujikuta unakwama na hata kushindwa kuendeleza biashara yako. Unapochagua aina ya bidhaa kwa ajili ya biashara yako ya mtandaoni, ni muhimu kuzingatia mambo makuu matatu:
Kuwa tofauti na wengine – Inawezekana kabisa kuuza kitu ambacho tayari wengi wanauza lakini unapojitofautisha, unawapa wateja kitu tofauti na hii inaweza kuwa chachu ya maendeleo yako. Unapokuwa mbunifu, bidhaa zako zinakuwa tofauti sokoni hivyo ni rahisi kwa wateja kushawishika na kununua kutoka kwako badala ya kwenda kwa wauzaji wengine. Aidha, sio lazima kuanza kwa kuuza bidhaa kubwa, unaweza kuanza kidogo kidogo na kufanya vizuri zaidi kwani wateja walio wengi ni watu wa chini na kati. Unapoteka kundi hilo, upo katika nafasi nzuri ya kufanikiwa.
Hakikisha unatatua tatizo – Unapowekeza katika biashara yoyote, ni muhimu kujiuliza je unarahisisha maisha ya watu? Angalia kama kuna tatizo katika jamii inayokuzunguka. Huu ni mwanzo mzuri ambao bila shaka utazaa matunda. Unapotatua tatizo katika jamii, una uhakika wa kuwa na wateja wa kudumu. Fikiria kama jamii yako ina uhaba wa wauzaji wa matunda, ukianzisha mradi wako na kuepusha watu kwenda umbali mrefu kwa ajili ya kufuata wanachohitaji, basi biashara yako ipo katika muelekeo sahihi. Kabla ya kuamua bidhaa unayotaka kuuza mtandaoni, jiulize bidhaa hii inatatua tatizo katika jamii? Kama ndio basi bila shaka itapokelewa vizuri.
Faida – Hiki ni kitu muhimu unapochagua aina ya biashara ya kufanya mtandaoni. Ni wazi kuwa biashara inahitaji fedha au faida kuendelea mbele hivyo fikiria kuuza bidhaa ambayo unajua inaweza kukuletea faida haraka hasa kama ndio kwanza umeingia katika sekta hii. Unahitaji kuingiza faida ili kujiendeleza zaidi na hii ni ngumu ikiwa utachagua kuuza bidhaa ambayo haizalishi faida moja kwa moja.
Ikiwa unafikiria kuanzisha biashara mtandaoni, ni muhimu kutathmini mambo hayo ili kuwa katika muelekeo sahihi. Biashara ni sekta yenye changamoto nyngi lakini unapojipanga vizuri, ni sekta ambayo inaweza kukufikisha mbali katika maisha.