Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIUJASIRIAMALI TUMIA WAZO LAKO KUWA AJIRA

TUMIA WAZO LAKO KUWA AJIRA

0 comment 157 views

Idadi kubwa ya watanzania wamejiajiri. Ujasiriamali umezidi kuwavutia watu wengi hasa vijana ambao baada ya masomo wamekuwa wakifikiria kujiajiri badala ya kutafuta ajira. Ili kufanikiwa katika shughuli yoyote ambao unatarajia kufanya jambo la muhimu kuliko yote ni kuwa na wazo zuri la biashara. Hata kama una mtaji wa kutosha huwezi kufika mbali kibiashara kama wazo lako halijitoshelezi. Wengi hushindwa katika hatua hii muhimu kuliko zote na kupelekea biashara zao kushindwa kusimama kwa muda mrefu. Hapo chini ni baadhi ya mbinu ambazo unaweza kutumia ili kupata wazo bora la biashara.

Kwanza kabisa inatakiwa kujenga biashara yako kutokana na ujuzi ulionao. Biashara kamwe haitofika juu kama unafanya kitu ambacho hauna uelewa nacho. Ni vizuri kujenga biashara yako kutokana na ujuzi na uzoefu ulionao. Kama unafahamu vizuri kuuza duka basi anzisha duka lako mwenyewe, kama ulishawahi kufanya kazi katika mgahawa basi anzisha wa kwako mwenyewe. Ni muhimu kuwa na uelewa wa kutosha wa kile unachotarajia kufanya kabla ya kusimamisha biashara yako.

Inapaswa kuangalia nini jamii inayokuzunguka inahitaji kabla ya kuanzisha biashara yoyote ile. Kufanya hivyo kutasaidia kufahamu ushindani uliopo, kujua jinsi ya kuvutia soko na pia kuangalia kama wazo lako linalipa mahali ulipo. Kama umezungukwa na biashara za mbogamboga na wewe ukafungua kitu hicho hicho hutakuwa na uhakika na biashara hiyo kwa sababu watu kumi tayari wanaifanya. Hivyo ni muhimu kuangalia ni nini jamii yako inakosa na kutengeneza wazo lako la biashara kutokana na mapungufu hayo.

ADVERTISEMENT

Angalia mfumo wa maisha ulivyo. Kama mjasiriamali unapaswa kufikiria kuwa watu wanaokuzunguka ndiyo wateja wako watarajiwa. Hivyo ni muhimu kuangalia maisha yao ya kila siku na kupata wazo lako kutokana na jinsi maisha yao yanavyoenda. Huwezi kuanzisha kibanda cha simu mahali ambapo unaona kila mtu anamiliki simu tayari sababu hakuna atakayehitaji huduma hiyo. Kama jamii yako ni ya maisha ya chini anzisha biashara ambayo wanaweza wakaimudu na siyo ambayo itakuwa juu ya uwezo wao wa kiuchumi. Kama umezungukwa na hospitali kwa mfano una nafasi nzuri ya kuanzisha duka ka madawa na kufaidika kutokana na mazingira kuwa rafiki kwa aina hiyo ya biashara.

Pia unaweza kuchukua wazo la biashara ambalo tayari lipo na kuliboresha kulingana na mahitaji ya eneo unalotarajia kufanya biashara yako. Watu wengi hutumia mbinu hii kwani ni rahisi kutambua nini hasa wanaweza kufanya kwa kuangalia nini wajasiriamali wengine wamefanya na kufanikiwa. Unaweza kuangalia mitandao ya kijamii au hata kupitia tovuti mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi na kuona biashara gani zimefanikiwa zaidi. Baadaye unaweza kuziboresha ili kukudhi mahitaji ya mazingira yanayokuzunguka.

Wazo la biashara ndiyo hatua ya awali kabisa na inahitaji kufanyiwa uchunguzi wa kina ili kufahamu ni nini hasa kinahitajika. Wazo lako ndiyo mtaji wako wa kwanza. Wekeza muda wa kutosha katika hatua hii na utaona matunda yake baadaye. Baada ya kupata wazo lenye tija kwako pamoja na jamii kwa ujumla ndipo unaweza kuanza kutafuta mtaji na kubadili wazo lako kuwa ajira yako.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter