Home VIWANDA Tutafanikisha Tanzania ya viwanda bila kilimo cha uhakika?

Tutafanikisha Tanzania ya viwanda bila kilimo cha uhakika?

0 comment 76 views

Ili kufanya kazi, viwanda vinahitaji malighafi za kutosha kuzalisha bidhaa ambazo baadae zitatumika kwa matumizi mbalimbali. Serikali ya awamu ya tano imejipanga kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa ni nchi itakayojijenga kiuchumi kupitia viwanda, jambo ambalo limepokelewa kwa mikono miwili na wadau wa maendeleo. Lakini tupo tayari kwa ajili ya hatua hiyo? Tuna malighafi ya uhakika? Sekta ya kilimo imejipangaje kufanikisha uchumi wa viwanda?

Lazima tukubali kuwa ili viwanda viwepo, lazima sekta ya kilimo iimarike. Lazima wakulima wetu wapatiwe elimu zaidi kuhusiana na kilimo bora na cha kisasa kwani walio wengi bado wanafanya kilimo cha kubahatisha. Lazima wakulima waachane na kilimo cha kutegemea mvua. Ili kufanikisha azma ya serikali ni lazima kuelekeza maofisa kilimo zaidi vijijini ili kuhakikisha kuwa wakulima kote nchini wanafikiwa na kupatiwa fursa za kukuza kilimo chao.

Viwanda haviwezi kuzalisha pasipo kuwa na malighafi ambayo inatokana na kilimo. Uwekezaji zaidi unatakiwa katika sekta hii ili kutengeneza mazingira bora zaidi ya uchumi wa viwanda. Sekta ya kilimo ikifanikiw kusimama imara basi viwanda navyo havitayumba kwani kutakuwepo na malighafi ya kutosha hivyo uzalishaji utaendelea bila matatizo. Unaweza kusema kuwa sekta hizi mbili ni kama mapacha. Zinahitaji kufanya kazi kwa pamoja. Hiyo basi kwanini tusielekeze nguvu zaidi kuboresha kilimo chetu?

Huu ni wakati muafaka wa kuwaelimisha wakulima kuhusu kilimo cha umwagiliaji, kilimo biashara, kufanya kilimo chao kwa kutumia teknolojia za kisasa na vilevile kuwapa kipaumbele katika masuala ya mikopo ili kuwezesha kasi ya kilimo kwenda sambamba na ile ya viwanda kwani kufanya hivyo kutawapa uhakika wa soko wakulima na vilevile kutawezesha viwanda kutekeleza majukumu ya uzalishaji pasipo tatizo lolote.

Kilimo ni sekta ambayo inaajiri watanzania wengi na inakadiriwa kuchangia takribani 23% ya pato la taifa ikiunganishwa na uvuvi na ufugaji. Hivyo basi changamoto zilizopo zikiendelea kutafutiwa suluhu, watu wengi zaidi wanaweza kupata ajira kupitia sekta hii na uwepo wa wakulima wengi zaidi unahakikishia uwepo wa viwanda vya kudumu hapa nchini ambavyo navyo vitazalisha ajira kwa kiasi kikubwa.

Sera hii ya uchumi wa viwanda itafanikiwa kwa asilimia mia moja endapo mapinduzi makubwa yatafanyika kuimarisha kilimo hapa nchini. Viwanda vinahitaji malighafi na malighafi hizo ni matokeo ya kilimo bora. Wakulima waelimishwe na watengenezewe mazingira ya kufanya kilimo cha kisasa ambacho kinatumia teknolojia kama ambavyo nchi zienye mafanikio katika kilimo zinafanya. Tukifanikiwa katika hili, basi bila shaka Tanzania ya viwanda nayo itawezekana.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter