Kituo cha utafiti wa kilimo nchini (TARI) kimechagua eneo la viwanja vya maonesho ya nane nane vilivyopo kata ya Nyakabindi wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu kuwa kituo endelevu cha uenezaji wa teknolojia lengo likiwa kuwawezesha wakulima kupata huduma za kilimo kwa mwaka mzima.
Hayo yamebainishwa na Bibi. Mshaghuley Ishika kutoka TARI Dodoma kwenye kikao cha maandalizi nane nane kilichofanyika Juni 15, 2020 kwenye jengo la mkoa wa Simiyu lililopo kwenye viwanja hivyo kikwahusiaha viongozi wa Kanda ya ziwa Mashariki (Simiyu, Mara na Shinyanga).
Aidha, Ishika amesema kituo hicho kitawarahisishia wakulima kupata bidhaa zinazozalishwa kwenye Kituo hicho ambapo kwa hapa nchini huzalishwa katika vituo 17, huku akibainisha kuwa TARI kwa kutambua hilo wameamua kuongeza eneo la vipando katika Viwanja vya Nyakabindi na kufikia hekari 3.
“Mbali na kuwa kituo endelevu cha usambazaji teknolojia kutakuwa vifaa na duka la mbegu zinazozalishwa na TARI ambazo zinapatikana katika vituo 17 hapa nchini na litamsaidia mkulima kujifunza mengi kuhusiana na kilimo; kituo hiki pia kimepatiwa mtumishi wa kudumu atakayekuwa anasambaza teknolojia kanda ya ziwa Mashariki ,” amesema Ishika.
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amesema maandalizi ya Maonesho ya Nanenane Kitaifa mwaka 2020 yamefikia 70% na kuongeza kuwa kwa upande wa vipando vimefikia 75%.
Wakati huo huo Sagini amewaomba viongozi wote wanaotoka kwenye mikoa inayounda kanda ya ziwa Mashariki (Simiyu, Mara na Shinyanga) wakiwemo wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji kuhudhuria kikamilifu kwenye vikao vya maandalizi ili yale wanayokubaliana wayatekeleze kwa wakati.
Akizungumzia masuala ambayo bado yanafanyiwa kazi Sagini amesema kwa sasa kamati ya maandalizi inaendelea na ni ukarabati wa miundombinu ikiwemo maji ,barabara na umeme huku akiwaomba washiriki kutoa michango yao mapema ili kufanikisha maandalizi kwa wakati.
Awali akimwakilisha mkuu wa mkoa wa Mara,Mhe.Adam Malima, Mkuu wa wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, ameuhakikishia umma kuwa Maonesho ya Nanenane mwaka 2020 yatakuwa bora zaidi na yataacha alama; kutokana na maonesho hayo kufanyika kitaifa kwa miaka mitatu mfululizo katika kanda ya ziwa Mashariki.
Katika hatua nyingine mhandisi Msafiri amezitaka halmashauri zote ambazo hazijaanza na zile ambazo maandalizi yake yanaenda taratibu, kuharakisha kusimamia maandalizi hayo na kuhakikisha yanakuwa ya kuridhisha, ili wakulima watakapokwenda kujifunza waone umuhimu wa kilimo chenye tija.
Kanda ya ziwa Mashariki inaundwa na mikoa mitatu ambayo ni Mara, Shinyanga na Simiyu na mwenyeji wa maonesho ya Nane nane kitaifa ni mkoa wa Simiyu kwa miaka mitatu mfululizo sasa, ambapo kwa mwaka 2020 kaulimbiu ya maonesho haya ni “KWA MAENDELEO YA KILIMO MIFUGO NA UVUVI CHAGUA VIONGOZI BORA 2020”.