Benki ya Stanbic imetwaa tuzo ya benki bora ya mwaka kwa kutimiza mahitaji ya wateja wake na kuwa dhabiti katika kipindi cha janga la ugonjwa wa corona.
Mkurugenzi Mkuu wa benki hiyo Kevin Wingfield alisema wamefanikiwa kupata tuzo hiyo kutokana na ushirikiano walioupata kutoka kwa wateja wao.
Vigezo vingine ambavyo vimechangia benki hiyo kupata tuzo ni pamoja na kuahirisha ulipaji wa mikopo wakati wa kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa corona na kuanzisha huduma maalum ya kuwasaidia wateja wake kuhimili katika kipindi cha COVID-19 ijulikanayo kama Africa China Agency Proposition (ASAP).
Wingfield alisema watahakikisha wanaendelea kujenga imani kwa wateja wao kama kauli mbiu yao ya mwaka huu inavyosema hususani kuongeza na kuchagiza maendeleo ya nchi.
“Tuzo hii ni kielelezo cha juhudi zetu katika kuchangia maendeleo ya Tanzania na maendeleo ya shughuli zinazofanywa na wateja wetu hususani katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi ukizingatia mwaka huu tunasheherekea miaka 25 ya uwapo wa Benki ya Stanbic nchini,” alisema.
Benki ya Stanbic ni sehemu ya Standard Bank Group ambayo ni benki kubwa Afrika kwa umiliki wa mali na inapatikana katika nchi 20 barani Afrika.