Home KILIMO Kilimo cha zao la mkonge kuokoa bilioni 577

Kilimo cha zao la mkonge kuokoa bilioni 577

0 comment 127 views

Tanzania itaokoa Sh. bilioni 577 zinazotumika kuagiza vifungashio nje ya nchi kila mwaka kwa kufufua zao la mkonge.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali imeingiza zao hilo katika orodha ya mazao nyeti ya kimkakati.

Amesema hadi sasa Tanzania ni mzalishali wa pili duniani wa mkonge ikitanguliwa na Brazil Ambato inazalisha tani 150,000 kwa mwaka.

Akizungumza katika kikao cha wadau wa zao hilo na kushirikisha wafanyabiashara, wakulima na viongozi kutoka mikoa mitano inayolima mkonge, Majaliwa alisema mpaka kufikia mwaka 2025, Tanzania inatarajia kuzalisha tani 120,000 kwa mwaka.

Majaliwa alisema Tanzania inatumia Dola za Marekani milioni 245 hadi 250 sawa na bilioni 577.277 kwa ajili ya kuagiza vifungashio kutoka nje ya nchi kila mwaka.

Alisema zao hilo ni miongoni mwa mazao ya biashara nchini ambayo mikakati yake ikitekelezwa vizuri, itawezesha serikali kupata fedha za kigeni na kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja.

Waziri Mkuu alisema serikali imeongeza zao la mkonge na mchikichi katika idadi ya mazao mkakati ambayo ni pamba, korosho, chai, tumbaku na kahawa.

“Kilimo cha mkonge na mchikichi kinatuondolea mzigo mkubwa na kupunguza gharama, mfano baada ya kuhamasisha kulima mchikichi, tunaokoa zaidi ya dola za Marekani milioni 470 kuagiza mafuta nje ya nchi,” alisema.

Aliziagiza halmashauri zote nchini kuhakikisha wanazalisha vitalu vya miche ya mkonge na kuwapatia wakulima.

Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe alisema wizara imeandaa utaratibu wa hati dhamana utakaowezesha wakulima wadogo kuchukua mkopo kwenye taasisi za fedha kwa riba ya asilimia mbili.

Akiongelea suala la mbegu alisema “kupitia taasisis zetu za utafiti ikiwemo ASA, TARI na TOSCI kumekuwa na uzalishaji wa mbegu ili kuongeza ubora wa miche na ubora wa zao la mkonge”.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mkonge Saadi Kambona alisema kwa sasa mkulima mdogo ndie anayeongoza uzalishaji kwa kuzalisha tani 9,728 kupitia mashamba ya bodi.

Aliwataja wazalishaji wengine kuwa ni Amboni anayezalisha tani 8,277 na Mohamed Enterprises anayezalisha tani 4,922.

Mikoa inayolima mkonge ni pamoja na Pwani, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Shinyanga na Mara.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter