Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetengeneza kanuni ndogo zitakazoratibu utoaji wa huduma za vifurushi vinavyotolewa na kampuni mbalimbali za simu nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Eng. James Kilaba amesema dhumuni la kupitisha kanuni hizo ndogo ambazo zinaanza April 02, 2021 ni kupunguza tofauti kubwa iliyokuwepo kati ya bei ya vifurushi na bei za kutumia huduma bila kujiunga na Vifurushi.
Miongoni mwa kanuni hizi ni mtoa huduma ataweka utaratibu au mfumo wa kumwezesha mtumiaji wa huduma kuhamisha uniti za kifurushi kwenda kwa mtumiaji mwingine ndani ya mtandao wake kwa masharti ya kiasi cha chini kuhamisha kitakuwa MB 250.
Mtoa huduma pia, atatakiwa kutoa taarifa kila wakati matumizi ya kifurushi yatakapifikia asilimia 75 kabla ya kuisha na asilimia 100 kitakapomalizika kabisa.
Nyingine ni huduma zote za vifurushi lazima zipate vibali vya TCRA huku mamlaka hiyo pia ikitoa mwongozo wa bei zilizowekwa na mamlaka hiyo.
Pia vifurushi vyote havitaondolewa au kurekebishwa ndani ya miezi mitatu baada ya kuidhinishwa.