Waziri wa kilimo Prof Adolf Mkenda amewahakikishia wawekezaji wa ndani wa viwanda vya kuzalisha viuatilifu vya mazao na mifugo kuwa serikali haitanunua biadhaa hizo nje ya nchi na badala yake watanunua vya ndani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kiwanda cha kuzalisha viuatilifu cha kampuni ya kimataifa ya usambazaji pembejeo nchini cha Bajuta kilichopo mkoani Arusha, Prof Mkenda amesema serikali italinda viwanda vya ndani vya bidhaa hizo kwa maslahi ya wawekezaji na wajasiriamali wa ndani.
Alisema serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kuagiza viuatilifu vya mazao na mifugo na kwamba iwapo wawekezaji wa ndani watazalisha bidhaa hizo kwa ubora unaotakiwa serikali haitasita kuvinunua.
“Serikali imekuwa ikitumia viuatilifu kwa ajili ya mazao kama korosho, pamba, kahawa na mazao mengine na fedha zinazotumika ni za wakulima na mbaya fedha hizo zinaenda nje ya nchini” alisema.
Waziri Mkenda alisema iwapo wawekezaji hao wataamua kuanza kuzalisha pembejeo za Kilimo na mifugo itaokoa fedha nyingi zinazoenda nje ya nchi na itapunguza gharama kwa wakulima.
“Naagiza taasisi zinazodhibiti ubora na taasisi nyingine kuchunguza ubora wa viuatilifu vinavyozalishwa hapa na kama vina ubora serikali haitoagiza nje kabla hatujamaliza vya ndani na tunaamini tukifanya hivyo pato la nchi litakuwa na kuboresha maisha ya watanzania ikiwemo wakulima.”
Akizungumzia ujenzi wa Kiwanda hicho, alisema uwekezaji huo utaleta tija na kusaidia huduma za viuatilifu kwa wananchi na kwamba hatua hiyo inaunga mkono jitihada za serikali za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo Gesso Bajuta amesema kiwanda hicho kinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu na kwamba kitazalisha zaidi ya lita milioni 4.5 kwa mwaka.