Home KILIMO Utekelezaji mipango ya kilimo ipewe kipaumbele: Majaliwa

Utekelezaji mipango ya kilimo ipewe kipaumbele: Majaliwa

0 comment 106 views

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha inaweka kipaumbele cha utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (DADPs) na kutafuta fedha zitakazowezesha utekelezaji wake.
Majaliwa ametoa agizo hilo Machi 2, 2022 wakati akizindua Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya (DADPs jijini Dodoma.

Pia amezitaka taasisi za fedha zijipange kutambua hati miliki za ardhi za wakulima kama dhamana ya kupata mikopo.
Amezielekeza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga fedha kutoka katika mapato yake ya ndani kwa ajili ya utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Wilaya.
“Kwa kuwa asilimia kubwa ya rasilimali za utekelezaji wa ASDP II zinalenga kuelekezwa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa waongeze usimamizi wa fedha na rasilimali,” amesema Waziri Mkuu.

Amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi Watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa wahakikishe wanajenga uwezo wa kusimamia utekelezaji wa miradi katika ngazi mbalimbali na kubuni vyanzo vingine vya mapato kuendeleza miradi ya kuendeleza kilimo.
Aidha, Majaliwa ameiagiza Ofisi ya Rais – TAMISEMI kupitia Halmashauri zote nchini ziendelee kutenga maeneo ili kuwawezesha wananchi kufanya shughuli za kilimo na shughuli nyingine kama vile ufugaji.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Innocent Bashungwa amesema watashirikiana na Wizara za Sekta ya Kilimo kutekeleza Mipango ya Maendeleo ya Kilimo ya Wilaya kwa kutafuta rasilimali fedha na kusimamia kikamilifu matumizi na utekelezaji wake pamoja na kuimarisha mifumo ya kiteknolojia ya habari na mawasiliano katika sekta ya kilimo (TEHAMA) na kuwezesha upatikanaji wa huduma za kifedha.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter