Home WANAWAKE NA MAENDELEO Tanzania: Tutaendelea kusimamia usawa, uwezeshaji wanawake

Tanzania: Tutaendelea kusimamia usawa, uwezeshaji wanawake

0 comment 34 views

Tanzania imezihakikishia nchi za Umoja wa Afrika kuendelea kusimamia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi katika sekta mbalimbali na kuwawezesha kupata fursa katika sekta hizo.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mwanaidi Ali Khamis ameeleza hayo mara baada ya kuwasili nchini akitikokea Ethiopia alikoshiriki Mkutano wa Sita wa Kamati Maalum ya Mawaziri ya Umoja wa Afrika wanaoshughulikia masuala ya Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake uliofanyika jijini Addis Ababa Ethiopia.

Mwanaidi amesema nchi za Afrika zimetoa msimamo na kauli moja ya kuhakikisha zinasimamia na kuzingatia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana kupitia Sera na Programu ya kukabiliana na maafa yanayosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi na mazingira.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa hatua mbalimbali za kutokomeza ukatili kwa wanawake na wasichana katika Mkutano huo amesema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuchukua hatua katika kutomeza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na wasichana na uwezeshaji kwenye nafasi za uongozi na kiuchumi.

Ameeleza kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika katika kutetea na kulinda maslahi na haki za wanawake na wasichana barani Afrika ili waweze kupata fursa mbalimbali katika uongozi na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Ameongeza kuwa miongoni mwa maazimio yaliyotokana na mkutano huo ni pamoja na nchi za Afrika kuwawezesha wanawake na wasichana katika masuala ya uongozi kwenye kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, kuongeza ufadhili na uwekezaji katika miradi ambayo inazingatia masuala ya jinsia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Aidha Mhe. Mwanaidi ameeleza kuwa lengo la mkutano huo wa Ethiopia ni kuhakikisha kuwa matokeo ya Mkutano 66 wa Kamisheni ya Wanawake Duniani yananufaisha wanawake na wasichana wa mijini na vijijini barani Afrika.

Pia ameyataja maazimio mengine ya Mkutano huo kuwa nchi za Afrika kuendelea kushirikiana na Asasi za kiraia, viongozi wa dini na sekta binafsi, viongozi wanawake na jamii kwa ujumla kuchukua hatua muhimu kwaajili ya kutokomeza ukatili kwa wanawake na wasichana,

“Katika hili Umoja wa Nchi za Afrika umezitaka nchi wanachama kuzindua Kampeni za kitaifa za kutokomeza ukatili kwa wanawake na wasichana zitakazosadia kutoa elimu kwa jamii kupambana na vitendo hivyo vinavyorudisha nyuma jithada za kuwaibua wanawake na wasichana katika sekta mbalimbali” amesema.

Aidha, mkutano huo umekubaliana kuanzishwa kwa mfuko wa Maendeleo ya wanawake barani Afrika (Trust Fund for Africa Women) utakaosadia kuwawezesha wanawake na wasichana katika nchi za Afrika kujikwamua kiuchumi kupitia mikopo itakayowawezesha kufanya bisahara na miradi mbalimbali katika maeneo yao.

Mkutano wa 6 wa Kamati Maalum ya Mawaziri ya Umoja wa Afrika wanaoshughulikia masuala ya Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake ni mwanzo wa Mkutano 66 wa Kamisheni ya Wanawake Duniani utakaofanyika jijini New York nchini Marekani kuanzia Machi 14, 2022.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter