Na Mwandishi wetu
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira amewashauri wafugaji jamii ya wamasai mkoani humo kupunguza idadi ya mifugo yao ambayo inasababisha uharibifu wa mazingira na migogoro ya ardhi kati ya kundi hilo na wakulima.
Mghwira ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi kutoka jamii ya kimasai katika Kata ya Mabogini Wilayani Moshi Vijijini. Ametaka jamii hiyo kufuga kwa kutumia mbinu za kisasa zaidi na kupunguza idadi ya mifugo waliyonayo.
Mbali na hayo, Mghwira pia amewataka viongozi wa vijiji kuandaa mikakati ambayo itasaidia wafugaji kuendelea kujiingizia kipato wakiwa na idadi ndogo zaidi ya mifugo kwani ongezeko la watu katika wilaya hiyo limepelekea uhaba wa ardhi.
Diwani wa Kata ya Mabogini Emmanuel Mzava amesema tayari utaratibu wa kutenga maeneo yaliyoshindwa kuendelezwa umeanza na wakati huo huo kamati maalum imeundwa ili kudhbiti makundi makubwa ya mifugo yanayoingizwa katika mashamba ya wakulima.