Unaweza usiamini lakini inawezekana, usiichukulie poa.
Biashara ya makopo ni biashara kama biashara zingine.
Watu wengi wanaofanya kazi ya kuokota makopo huonekana kama wamechanganyikiwa kutokana na muonekano wa baadhi yao, wengi wakionekana wachafu.
Usichokijua ni kwamba biashara hii ina uwezo wa kukupatia kipato cha hadi shilingi 20,000 kwa siku.
Khalid Juma, mnunuzi wa makopo eneo la Kimara jijini Dar es Salaam anasema kwa siku wapo waokota makopo ambao huingiza hadi Shilingi 20,000 kwa kuuza makopo.
Anaeleza kuwa kilo moja ya makopo hayo huuzwa kwa shilingi 400, hivyo mtu ukiweza kupata kilo 50 za makopo hayo, basi hupata Shilingi 20,000 kwa siku.
Hicho ni kiwango cha juu ambacho muokota makopo anaweza kukifikia.
“Watu wanawadharau waokota makopo, lakini nikwambie kuna watu hapa wanapata hadi Shilingi 20,000 kwa siku kwa makopo haya haya unayoyaona. Mtu anaokota makopo hadi Kilo hamsini kwa siku,” anaeleza.
Anaeleza kuwa juhudi ya mtu kuokota au kukusanya makopo mengi ndiyo humwezesha kupata fedha zaidi kwani wao kama wanunuzi hawana kiwango cha mwisho cha kununua.
“Yani hapa ni mtu akiweza hata kuleta kilo mia moja ni yeye tuu, sisi tunanunua na yakifika kiwango fulani, basi huwa yanakuja kuchukuliwa na kupelekwa kwa wanunuzi wakubwa (kiwandani) kwa ajili ya kuchakatwa,” anasema Juma.
Mmoja wa waokota makopo eneo la Kimara anasema kazi hiyo ina changamoto mbalimbali ikiwemo kuonekana kama watu waliochanganyikiwa katika jamii.
“Watu wanatuona kama tumechanganyikiwa (vichaa) kwani kuokota makopo au taka vichaa ndio hufanya hivyo, lakini kwa sasa makopo haya ni dili na ndio maana unaona tunaifanya kama kazi zingine tuu.”
Akiongelea suala la kuwa wachafu anasema mazingira ya kazi hiyo huwafanya wengi wao kuwa wachafu na kutoonekana nadhifu.
“Wakati mwingine tunapita kwenye majalala na sehemu mbalimbali ambazo mtu huwezi kuwa msafi ndio maana tunaonekana hivi tulivyo,” amesema.
Wananchi mbalimbali wametoa maoni yao kuhusiana na biashara ya makopo na watu wanaookota makopo hayo.
Nancy Kimario, mkazi wa Kimara anasema “hawa waokota makopo kweli wanasaidia kuondoa hizi taka za plastiki mitaani lakini baadhi yao huonekana kama vibaka na wezi kutokana na jinsi walivyojiweka kimuonekano.
Unakuta una makopo nyumbani lakini unapomuita kuyachukua anaanza kuangalia huku na kule kama mtu anayetafuta kitu cha kuiba, yani wakati mwingine wanatia shaka kwa kweli.”
“Kweli ni biashara tuu na mtu ukiitilia maanani unajipatia kipato sio sawa na kukaa bure, lakini baadhi ya hawa waokotaji wa haya makopo wakishauza tuu wanakimbilia kununua pombe tena hizi za bei rahisi yaani ukiwaona huko barabarani ni kama mateja, unaogopa hata kumuita kama una makopo nyumbani,” amesema Shadia mkazi wa Kimara Stop Over.