Home BIASHARA Serikali ya Tanzania yazuia uingizaji wa vifaranga

Serikali ya Tanzania yazuia uingizaji wa vifaranga

0 comment 130 views

Serikali ya Tanzania imezuia uingizaji wa vifaranga vya kuku kutoka nje ya nchi ifikapo July 30, 2022.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amesema ifikapo Julai 30 hakuna vifaranga vya kuku vitakavyoingizwa nchini na kwamba serikali haitatoa tena vibali vya kuingiza vifaranga hivyo.

Ulega alisema lengo ni kulinda soko la ndani pamoja na kuwepo kwa mfumo wa taarifa zinazohusu wazalishaji wa vifaranga vya kuku kuanzia wazalishaji wakubwa hadi wadogo ambao wamesajiliwa na kutoa taarifa serikalini ili kuiwezesha kujua kiwango cha uzalishaji na takwimu sahihi kuhusu mahitaji ya vifaranga nchini sambamba na kuzuia vifaranga visivyo na ubora.

Ulega alieleza hayo jijini Dodoma wakati wa kikao cha wizara na wadau wa tasnia ya kuku kilicholenga kujadili namna ya kukuza tasnia hiyo na utekelezaji wa sheria ya mwaka 2006.

Akifungua mkutano huo uliojikita katika upatikanaji wa vifaranga vya kuku, chakula na bei ya sokoni, Ulega alisema ni mategemeo kuwa serikali haitaona vifaranga vinaingizwa nchini kutoka nje ya nchi.

Serikali imekuwa ikizuia uingizaji wa vifaranga kutoka nje ya nchi ili kudhibiti ugonjwa wa mafua ya ndege kwa mifugo jamii ya ndege na kulinda wazalishaji wa kuku ndani ya nchi.

Wazalishaji wengi wa ndani huuza vifaranga kwa wastani wa Tsh 2,000 huku vifaranga kutoka nje vikiuzwa kwa Tsh 1,200.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter