Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameahidi ujenzi wa kiwanda cha kuchakata parachichi katika mkoa wa Iringa ili kuliongezea thamani zao hilo.
Kiwanda hicho kitajengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni tatu.
Akizungumza na wananchi wa eneo la Nyololo wakati wa ziara ya siku tatu mkoani humo Agosti 11, 2022 Rais Samia amesema kiwanda hicho kinajengwa kutokana na maombi aliyokuwa amepewa.
Rais Samia amesema “najua Iringa na Njombe ni wakulima wa maparachichi, kile kiwanda ambacho mbunge aliomba kisimamishwe kinabaki hapa. Na kule Njombe wameomba cha kwao tutawajengea.”
“Lengo ni kusafirisha maparachichi mengi zaidi yenye hadhi nzuri ili tupate pesa nyingi zaidi,” amesema Rais Samia.
Kwa sasa, Tanzania inapata takribani Dola za Marekani milioni 12 kwa mwaka kutokana na mauzo ya parachichi nje ya nchi.