Na Mwandishi wetu
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimezindua ripoti yake ya haki za binadamu na biashara kwa mwaka 2016 ambapo imebainika kuwa kuna changamoto katika utendaji kazi wa kampuni, ukiukwaji wa haki za binadamu ambazo kwa namna moja ama nyingine huathiri jamii pia, utendaji wa vyombo vinavyosimamia biashara na kutoa tathmini ya haki ya kumiliki ardhi na maliasili.
Mkurugenzi wa kituo hicho, Dk. Hellen Kijo-Bisimba amefafanua kuwa utafiti umeonyesha kuna ukiukwaji wa sheria, jambo linalopelekea ugumu katika kuhakikisha wafanyakazi wanafanya shughuli zao katika mazingira bora.
Mbali na hayo, Dk. Hellen ameeleza kuwa bado wameendelea kupata matukio ya ukosefu wa ajira stahiki hasa katika sekta ya viwanda. Ameongeza kuwa ajira ya ulinzi nayo pia bado ni changamoto kwani watu wameendelea kufukuzwa kazi pasipo taratibu maalum kufuatwa.
Ameshauri serikali kuangalia upya suala la ajira na mazingira ya wafanyakazi wa viwandani kwani bila kundi hili la watu, dhamira ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda haiwezi kutimia.