Rais Samia Suluhu Hassan amezindua mradi wa vihenge na maghala ya kuhifadhia nafaka mkoani Manyara wenye thamani ya bilioni 19.
Vihenge na maghala hayo yana uwezo wa kuhifadhi tani 40,000 za nafaka.
Akizungumza kabla ya kuzinduliwa kwa maghala hayo, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema ujenzi wa mradi huo ni mpango mkakati wa serikali katika kuboresha hifadhi ya chakula.
Bashe alisema maeneo matatu yamejengwa vihenge na maghala ya kuhifadhia chakula ambayo ni Manyara, Rukwa na Katavi ambapo kwa ujumla maeneo hayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi nafaka tani 90,000.
Kwa mujibu wa Waziri Bashe, hivi sasa nchi ina maghala ya kuhifadhi nafaka tani 250,000 na kuwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa vihenge na maghala yote uwezo wa hifadhi utafikia tani 341,000.
Bashe alisema malengo ni kuwa ifikapo Desemba 2023, nchi iweze kuhifadhi nafaka tani 500,000 na kuwa vihenge na maghala hayo yamejengwa kwa teknolojia ya kisasa ya kuondoa unyevu kwenye nafaka ili kuzuia sumu kuvu.
Alisema “lengo letu ni kwamba Aprili mwakani Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) waanze kununua mahindi kwa wakulima, mitambo ni ya kisasa hata kama nafaka zina unyevu, hukaushwa na kuzuia sumu kuvu.”