Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeishauri Wizara ya Maliasili na Utalii iendelee kuzifanyia maboresho kanuni na taratibu za uwekezaji kwenye maeneo ya Hifadhi za Taifa ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka ndani na nje ya nchi hali itakayoongeza ajira na Pato la Taifa.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Ally Juma Makoa (Mb) amesema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao na Semina kuhusu utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Wizara hiyo na maendeleo ya uwekezaji wa huduma za malazi katika maeneo ya Hifadhi za Taifa hapa nchini.
Amesema uwepo wa mazingira rafiki ya uwekezaji utawawawezesha wafanyabiashara wengi zaidi waendelee kuwekeza kwa kujenga hoteli jambo litakaloongeza uwezo wa Tanzania kupokea watalii wengi zaidi kwa wakati mmoja na kupunguza changamoto ya upungufu wa vyumba vya kulala wageni.
Aidha, ameishukuru Wizara hiyo kutoa semina kwa wajumbe wa Kamati hiyo akieleza kuwa imeongeza uelewa juu ya uwekezaji katika maeneo ya hifadhi.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) amesema Serikali inaendelea kuweka utaratibu mzuri utakaorahisisha uwekezaji katika Sekta ya Utalii kwa kuendelea kuifungamanisha mifumo yote inayotoa huduma na taarifa za uwekezaji ikiwemo ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Uhamiaji pamoja na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) ili iweze kusomana na kubadilishana taarifa.
“Kuna baadhi ya mifumo ya taasisi zetu inasomana na NIDA, Uhamiaji, BRELA na TRA na hii inarahisisha kujua taarifa za mwekezaji kama uraia wake, usajili wa biashara na hali ulipaji wa kodi,” amesisitizi Balozi Dkt. Chana.
Aidha, ameishukuru Kamati hiyo kwa kutoa ushauri na maoni na michango mbalimbali itakayoiwezesha Wizara ya Maliasili na Utalii kuboresha huduma mbalimbali katika Sekta ya Utalii.
136