Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amezindua Baraza la Chuo cha Taifa cha Sukari na kulitaka Baraza hilo kuhakikisha kuwa inakuwa Kituo cha Umahiri cha kuboresha sekta ya sukari nchini.
Katika uzinduzi huo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Wizara ya Kilimo-Dodoma na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli, Bashe amelitaka Baraza hilo kuhakikisha linatanua zaidi utendaji kazi wa chuo kutoka kuwa cha kuwafundisha wanafunzi na kuwa nguzo muhimu ya mabadiliko ya sekta ya sukari.
“Chuo hiki kinatakiwa kuwa Kituo cha Umahiri, kiwe ndio mahala pa kuchangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya kilimo cha miwa.
Nataka kiwe kina uwezo wa kusaidia katika kuongeza thamani ya sukari, kisaidie mbinu za kibunifu kwa kampuni za sukari ili zizalishe sukari ya matumizi ya kawaida na ya viwandani, kisiwe chuo tu kwa ajili ya wanafunzi peke yake” amesema.
Aidha, ameliagiza Baraza hilo kuhakikisha kuwa chuo kinafanya kazi kwa ukaribu na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI) na wadau wengine katika kilimo kuhakikisha wakulima wadogo na wakubwa wa miwa wanalima kwa tija.