Umewahi kuona mvinyo wa majani ya mlonge na asali?
“Huu ni mvinyo (wine) uliotengenezwa kwa majani ya mlonge na asali. Mvinyo huu huvundikwa kiasili kwa muda wa mwezi mmoja hadi miezi mitatu,” anaeleza Bahati Malangalila, Mkurugenzi wa One Love Naturals.
Malangalila ambae awewahi kufanya kazi kwa miaka 15 katika Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), sasa amejiajiri na anatengeneza bidhaa mbalimbali za asili ikiwemo mvinyo.
“Wakati nafanya kazi SIDO nilipata fursa ya kutembelea nchi mbalimbali ikiwemo China.
Kule China nilipata mafunzo ya uchachushaji (fermentation) na nikapata wazo la kutengeneza mvinyo.
Amesema baada ya kurejea nchini aliendelea na kazi ambapo baada ya muda wa miaka miwili aliacha kazi ili aweze kujiajiri.
“Wazo langu lilikuwa limejikita sana katika uchachushaji, na mwaka 2014 nilienda nchini Msumbiji na kuangalia hali za bidhaa huko.”
Malangalila ambae ana kiwanda cha kutengeneza mvinyo huo huko Kibaha kwa Mfipa mkoani Pwani, amebainisha kuwa alianza kutengeneza mvinyo huo hapa nchini mwaka 2021.
“Mvinyo huu unatengenezwa kwa njia ya asili kwa kutumia majani ya mlonge na asali, huu mvinyo ninaweza kuuita mvinyo lishe, na unywaji wake ninamshauri mnywaji kutumia kiasi kidogo” anaeleza Malangalila.