Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeingia makubaliano ya kujiunga na kamati ya mamlaka za usimamizi wa bima, masoko ya fedha na taasisi za fedha zisizo za kibenki (CISNA).
Naibu Gavana wa BoT, Usimamizi na Uthabiti wa Sekta ya Fedha Sauda Msemo amesaini makubaliano ya kujiunga na kamati hiyo kwa niaba ya BoT katika mkutano wa CISNA wa mwaka wa 46 huko Swakopmund, Namibia.
CISNA ni kamati inayoripoti taarifa zake kwa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji kupitia Kamati kuu ya Hazina ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Taarifa ya BoT inaeleza kuwa jukumu kuu la CISNA ni kuoanisha usimamizi wa huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi zisizo za kibenki katika nchi wanachama wa SADC sawasawa na viwango vya kimataifa ambavyo vinawekwa na taasisi husika za kimataifa.
“Kama msimamizi wa sekta za hifadhi ya jamii na taasisi za kifedha zisizo za kibenki, zikiwemo zinazotoa huduma ndogo za kifedha, BoT inawajibika kuwa mwanachama wa CISNA.
Kwa kujiunga na kamati hiyo ya CISNA, BoT itanufaika kupata uzoefu wa taasisi zingine za udhibiti na usimamizi katika nchi wanachama wa SADC na hivyo kufikia viwango vinavyotakiwa na kukubalika kimataifa,” inaeleza taarifa hiyo.