Home BENKI BoT yatoa ufafanuzi kuongezeka kwa riba

BoT yatoa ufafanuzi kuongezeka kwa riba

0 comment 324 views

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema mwenendo wa Uchumi wa Dunia ulikuwa unaashiria uwepo wa Mfumuko wa bei kwa siku za mbele, hivyo ikaona ni vema iongeze Riba ya Benki Kuu (Central Bank Rate-CBR) kutoka asilimia 5.5 kwenda asilimia 6.

BoT imeeleza hayo katika mkutano na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kutoa elimu kuhusiana na mfumo mpya wa sera ya fedha unaotumia Riba ya Benki Kuu (CBR) pamoja na uamuzi wa Kamati ya Sera ya Fedha kupandisha riba hiyo kutoka asilimia 5.5 hadi 6.

Riba mpya ya Benki Kuu itatumika katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2024 kuanzia mwezi April.

Akizungumza katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi, Dkt. Suleiman Missango, ameeleza kuwa Riba ya Benki Kuu hutolewa kama riba elekezi kwa mabenki kuweza kukopa fedha kutoka Benki Kuu.

“Ni riba ambayo BoT inatoa kama riba elekezi kwa mabenki kuweza kukopa fedha Benki Kuu ili ziweze kufanyia shughuli zao, ikiwemo kukopesha,” ameeleza.

Ameongeza kuwa riba hiyo hutumika pia kudhibiti mfumuko wa bei kwa kudhibiti kiwango cha fedha kilichopo kwenye mzunguko

“Benki Kuu ikiona kiwango cha fedha kilichopo katika uchumi kinaelekea kuwa zaidi ya pale kinapotakiwa, hutumia mfumo huu ili kudhibiti mfumuko wa bei kwa kupunguza ukwasi kwenye mzunguko,”

Vilevile, Mkurugenzi huyo wa BoT, ameeleza kuwa mfumo wa sera ya fedha unaotumia Riba ya Benki Kuu unasaidia mabenki na taasisi nyingine za fedha kupanga viwango vyao vya riba na sio kuweka ukomo wa riba kwa mabenki na taasisi zinazotoa mikopo.

“Kwa sababu hii ni riba elekezi, inasaidia mabenki na taasisi nyingine za fedha kuweza kupanga viwango vyao vya riba.

Mwanzoni wakati tunaanza kutumia mfumo huu watu walifikiri kuwa Benki Kuu inaenda kuweka ukomo wa riba, si kweli,” amesema.

Akitoa taarifa ya kuongezeka kwa Riba hiyo, iliyotangazwa Aprili 4, 2024 Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania Emmanuel Tutuba, alisema uamuzi wa kupandisha riba umetokana na maoteo au uchambuzi uliofanyika mwezi Machi 2024 ambao ulionesha kwamba endapo kiwango cha riba kingebakia asilimia 5.5, kulikuwa na viashiria vya mfumuko wa bei kuongezeka.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter