Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema moja ya mashirikiano katika Mkataba uliosania na Wizara pamoja na Huawei Tanzania ni kuongeza ushiriki wa wanawake katika TEHAMA.
Waziri Nape ameyasema hayo wakati akizungumza na Vyombo vya Habari mara baada ya kumalizika kwa sherehe za kutoa tuzo kwa washindi wa progamu ya ‘Seeds for the future’ inayotolewa na Huawei kwa kushirikiana na Vyuo Vikuu Tanzania.
“Takwimu za kidunia zinaonyesha ushiriki wa wanawake katika TEHAMA sio mzuri na mimi leo nimetoa wito kwao wawekeze kwenye maendeleo ya mtoto wa kike wa Kitanzania ili aone kwamba eneo la Teknolojia ni eneo ambalo anapaswa kwenda,” amesema Waziri Nape.
Amesema “na sasa hivi Dunia inakwenda katika ulimwengu wa Akili Bandia (AI), tunataka tushirikiane nao katika hayo maeneo na tunataka Watanzania wajue hayo maeneo vizuri na mtaona hii leo nimetoa wito wa kutafuta namna ambavyo ushiriki wa wananwake utaongezeka katika TEHAMA.”
“Sisi kama Wizara tumeona tunayo haja ya kuongeza mashirikiano kati ya sehemu hizi mbili za Wizara na Huawei Tanzania na pia tuliona namna TTCL walivyoshirikiana na Huawei Tanzania katika kupeleka intaneti ya kasi katika kilele cha mlima Kilimanjaro na hii imethibitisha kwamba Sekta binafsi na Sekta ya Umma zikishirikiana kwa matokeo yake ni makubwa” amesema Waziri Nape.
Katika hatua nyingine Waziri Nape ametoa rai kwa Watanzania kuendana na kasi ya Teknolojia ya Akili Bandia (Artificial Intelligence) kwani ni kitu ambacho hakikwepeki na imekuwa ikibadilika kila siku.
Sherehe hizo ziliambatana na kusaini Mkataba wa Makubaliano kati ya Serikali kupitia Wizara hiyo pamoja na Kampuni ya Huawei Tanzania pamoja na kuwatunuku vyeti wahitimu wa mafunzo hayo.