Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza riba ya asilimia 5.5 kwa robo ya kwanza ya mwaka huu ili kutimiza malengo ya kiuchumi katika kipindi hicho.
Riba hiyo imetangazwa kutokana na kikao cha Kamati ya Sera ya Fedha iliyokutana Januari 18, 2024.
Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba amesema kiwango hicho cha riba kilichotangazwa kinaendana na malengo ya kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unabakia ndani ya lengo la asilimia 5 na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kufikia lengo la asilimia 5.5 au zaidi kwa mwaka 2024.
Aidha amesema riba hiyo imezingatia lengo la kuhakikisha thamani ya Shilingi dhidi ya fedha za kigeni inaendelea kuwa imara.
“Ili kuwezesha kufikiwa kwa malengo haya, Benki Kuu itatumia nyenzo mbalimbali za sera ya fedha kuhakikisha riba katika soko la fedha baina ya benki hapa nchini (interbank market) inakuwa tulivu.
Benki Kuu itakuwa inafuatilia mwenendo wa riba ya mikopo ya siku saba katika soko hilo na kuchukua hatua kuhakikisha mabadiliko ya riba yanakuwa ndani ya wigo usiozidi asilimia 2 chini au juu (+/-2%) ya Riba ya BoT,” amesema Gavana Tutuba.
Ameeleza kuwa tamko hilo la Kamati ya Sera ya Fedha ni la kwanza kutolewa tangu Benki Kuu ya Tanzania ilipoamua kubadili mfumo wa utekelezaji wa sera ya fedha kutoka kutumia ujazi wa fedha na kuanza kutumia mfumo wa riba kuanzia Januari mwaka huu.
“Mfumo wa kutumia riba unatarajiwa kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa Sera ya Fedha.
Aidha, mabadiliko haya yanaendana na makubaliano ya Itifaki ya Kuanzisha Umoja wa Fedha wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikiwa ni mojawapo ya hatua kuelekea kuwa na Sarafu Moja na Benki Kuu Moja ya Afrika Mashariki.
Tanzania inakuwa nchi ya nne katika jumuiya kutumia mfumo wa riba, zingine ni Kenya, Uganda na Rwanda.
Riba ya Benki Kuu kwa robo ya pili ya mwaka 2024 itatangazwa mwezi Aprili mwaka huu. Hii ni kulingana na kalenda ya mikutano ya Kamati ya Sera ya Fedha itakayotolewa hivi karibuni.
Soma: BoT kuanza kutumia mfumo wa riba utekelezaji sera ya fedha