Home FEDHABIMA Watanzania watakiwa kutunza nyaraka muhimu kurahisisha ulipaji fidia

Watanzania watakiwa kutunza nyaraka muhimu kurahisisha ulipaji fidia

0 comment 213 views

Serikali imewataka wananchi kutunza kumbukumbu na nyaraka muhimu za rejea ili kuondoa usumbufu na kurahisisha zoezi la ulipaji fidia hususan kwa wasimamizi wa mirathi kupitia bima walizokata.

Wito huo umetolewa bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akijibu swali la Mbunge wa Muleba Kusini Dkt. Oscar Kikoyo, aliyetaka kufahamu wakati ambao Serikali itarekebisha Sheria ya Bima ya Tanzania ili kuweka kima cha chini cha malipo ya fidia kwa waathirika wa ajali za barabarani.

Waziri Dkt. Nchemba amesema kuwa Septemba 2022, Mamlaka ya Bima Tanzania ilitoa Mwongozo unaotambulika kama Mwongozo wa Viwango Elekezi vya Fidia ya Bima kwa madai ya majeraha ya mwili na vifo kwa mtu wa tatu kutokana na ajali za vyombo vya moto.

“Mwongozo huo wa Viwango vya Fidia ya Bima ulitolewa kwa mujibu wa Kifungu cha 6 na 11 cha Sheria ya Bima Sura Na. 394, lengo likiwa ni kuweka usawa na ubora katika ulipaji fidia zitokanazo na madai ya bima”, alisema Dkt. Nchemba.

Amesema kuwa utekelezaji wa mwongozo huo umepunguza kwa sehemu kubwa malalamiko kutoka kwa waathirika wa ajali za vyombo vya moto kwa kuwa kuna usawa katika suala la viwango vya fidia vinavyotolewa na kampuni za bima.

Aidha ameeleza kuwa Serikali itaendelea na jitihada za kujenga uelewa kwa wadau wa tasnia ya bima na wananchi kwa ujumla ili kutimiza matakwa ya Sheria ya Bima, Sura 394, ikiwemo kuboresha huduma za bima na kumlinda mteja.

Kwa upande mwingine, akijibu swali la Mbunge wa Konde Mohamed Said Issa kuhusu mkakati wa Serikali wa kuongeza mapato ya biashara zinazofanyika kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, Dkt. Nchemba amesema kuwa Serikali za pande mbili zimeendelea kuboresha na kutekeleza mikakati mbalimbali kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu mbalimbali za uwekezaji na biashara.

Ameeleza kuwa baadhi ya mikakati iliyotekelezwa ni pamoja na kuboresha na kuunganisha mifumo ya kodi ya Electronic Fiscal Device Management System (EFDMS) na Virtual Fiscal Management System (VFMS) ili kusomana na kurahisisha utozaji kodi, ada na tozo, kuboresha mifumo ya urejeshaji wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kurahisisha mifumo ya utoaji vibali, leseni na ukaguzi wa mizigo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter