Home Elimu Wakaguzi wa ndani Afrika watakiwa kubadilishana uzoefu

Wakaguzi wa ndani Afrika watakiwa kubadilishana uzoefu

0 comment 269 views

Wakaguzi wa Ndani barani Afrika wametakiwa kubadilishana uzoefu na kutumia teknolojia katika kutatua changamoto mbalimbali katika taaluma yao na kuhakikisha wanasaidia taasisi na Serikali zao kuboresha ufanyaji kazi ili kuchochea maendeleo.

Hayo yameelezwa jijini Arusha na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Saada Mkuya Salum, wakati wa Mkutano wa 10 wa Wakaguzi wa Ndani Barani Afrika, ulioanza kwa mikutano midogo inayofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Dkt. Mkuya amesema kuwa mkutano huo umewakutanisha wakaguzi kutoka nchi 27 za Afrika na kwamba mkutano huo ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu ambapo wageni watajifunza Tanzania na wageni watajifunza kwa wenzao kwa kuwa mazingira ya ukaguzi yamebadilika kutokana na kuimarika kwa teknolojia duniani.

‘’Tumezoea kuona ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu (CAG) lakini kuna wakaguzi wa ndani ambao wanafanya kazi kila siku ambao husimamia taratibu za matumizi ya fedha, utawala na mifumo hivyo mawanda yao ni mapana katika masuala ya ukaguzi na mkutano huu ni muhimu sana kwa nchi”, ameeleza Dkt. Mkuya.

Amebainisha kuwa Kada ya ukaguzi wa ndani watu wengi hawaielewi hivyo mkutano huo utasaidia kujua mamlaka ya mkaguzi, maadili na taratibu za kufuata ili kuwa na ufanisi katika utendaji kazi.

Aidha, Dkt. Mkuya amesema mkutano huo utafuatiwa na mkutano Mkuu utakaofunguliwa Aprili 17 mwaka huu na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdory Mpango.

Kwa upande wake Rais wa Taasisi ya Ukaguzi Tanzania (IIA Tanzania), Dkt. Zelia Njeza, amesema kuwa mkutano wa 10 wa Wakaguzi wa Ndani Afrika umehudhuriwa na Bodi ya Wakurugenzi wa Ukaguzi Duniani (IIA Global) ambao kabla ya mkutano huo wa 10 walikuwa na Kikao chao cha Bodi, jijini Arusha.

Amesema kuwa ni kwa mara ya kwanza katika historia ya IIA Global kuwa na mkutano wao wa Bodi Afrika hivyo Tanzania inajivunia kupata ujio huo ambao unafaida kwa kada ya ukaguzi lakini pia katika sekta ya utalii.

Dkt. Zelia amesema kuwa mkutano huo unategemea kuwa na washiriki zaidi ya 1,000 na kati yao washiriki 300 ni wageni kutoka nchi za Afrika na nje ya Afrika

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter