Home VIWANDANISHATI Nchi za Afrika zapewa wito matumizi nishati safi ya kupikia

Nchi za Afrika zapewa wito matumizi nishati safi ya kupikia

0 comment 8 views

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa wito kwa nchi za Afrika kutafuta njia na mikakati ya kuboresha uchumi na maisha ya wananchi wake kwa kutumia nishati safi ya kupikia ikiwa ni hatua pia ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya Tabianchi yanayochangiwa na uharibifu wa mazingira.

Dkt. Nchemba ametoa wito huo mjini Antananarivo nchini Madagascar kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati akihutubia katika Mkutano wa Mwaka wa Wanahisa wa Taasisi ya Africa50 (General Shareholders Meeting – GSM) na Jukwaa la Miundombinu la Afrika (Infra for Africa Forum meeting) Taasisi ambayo Tanzania ni mwanachama uliofanyika Septemba 19, 2024, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Ivato uliofunguliwa na Rais wa Nchi hiyo, Andry Rajoelina.

Aidha, Dkt. Nchemba amezishauri nchi hizo kuwekeza katika kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa wananchi wao kutumia nishati safi ya kupikia pamoja na faida zinazoambatana na utunzaji wa mazingira kiuchumi na kijamii.

Dkt. Nchemba pia ametoa wito kwa taasisi za fedha na sekta binafsi kushiriki katika kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi iliyosindwa, nishati ya jua, umeme wa joto ardhi, biogas, kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha na pia kuzalisha vifaa ama majiko yanayotumia nishati hiyo.

Katika msafara huo, Dkt. Nchemba ameambatana na Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Fedha za Umma (Public Finance Management) Amina Khamis Shaaban na Balozi wa Tanzania nchini Madagascar Faustine Kasike, mwenye makazi yake Mjini Maputo nchini Msumbiji.

Mkutano wa Wanahisa wa Africa50, umewakutanisha wadau mbalimbali kutoka Bara la Afrika na duniani kwa ujumla wakiwemo wawekezaji kutoka Taasisi za Umma na Sekta Binafsi, wakopeshaji, wataalam wa ujenzi wa miundombinu na kuwawezesha kutafuta suluhisho la changamoto za miundombinu katika Bara la Afrika pamoja na kukabikliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhimiza kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuchochea uchumi na maendeleo ya nchi hizo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter